28 June 2012

Uchaguzi Yanga ngoma nzito


Na Elizabeth Mayemba

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji ambaye anagombea nafasi ya Mwenyekiti katika Uchaguzi Mdogo wa klabu ya Yanga na Yono Kevella anayegombea nafasi ya Makamu na Ujumbe, wamewekewa pingamizi kwenye Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Uchaguzi huo wa kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu, unatarajiwa kufanyika Julai 15, mwaka huu.

Awali wagombea hao waliwahi kuwekewa pingamizi katika Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, lakini pingamizi hizo zikatupiliwa mbali na kamati hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema ni wagombea wawili tu ambao waliwekewa pingamizi na juzi ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha pingamizi hizo za wagombea.

"Manji na Kevella ndiyo waliowekewa pingamizi, hivyo tutaiachia Kamati ya Uchaguzi ya TFF ili kuzipitia pingamizi hizo," alisema Wambura.

Alisema Kamati hiyo ya TFF, inatarajiwa kukutana Julai 2, mwaka huu saa nne asubuhi kwa ajili ya kupitia pingamizi hizo baada ya hapo majina ya wagombea wote yatatajwa kwa ajili ya kuanza kampeni.

Kampeni za wagombea, zitaanza Julai 3, mwaka huu kwa kila mmoja kunadi sera zake juu ya nini atafanya akishinda.

Wagombea wengine katika kinyang'aniro hicho mbali na Manji na Kevella katika nafasi ya Mwenyekiti ni Sarah Ramadhan, John Jembele na Edgar Chibula huku Ayoub Nyenzi na Clement Sanga wakiwania Makamu Mwenyekiti.

Katika nafasi za ujumbe ni Lameck Nyambaya, Ramadhan Kampira,  Abdallah Bin Kleb, Ramadhan Said, Edgar Fongo, Ahmed Gao, Beda Tindwa, Jumanne Mwammenywa na George Manyama.

Wengine ni Gadeuncius Ishengoma, Aaron Nyanda, Omary Ndula, Shaban Katwila, Justine Baruti na Peter Haule.

No comments:

Post a Comment