27 June 2012

Mwanafunzi abakwa, kuuawa kikatili


Na Theonestina Juma, Bukoba

MWANAFUNZI wa kike anayesoma kidato cha pili Shule ya Sekondari ya Kaagya, mkoani Kagera, Advea Makanyaga (16), ameuawa kikatili kwa kunyongwa shingo, kuvunjwa taya kwenye shavu la kulia, kubakwa na mwili wake kutupwa shimoni.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Phillip Kalangi, alisema tukio hilo limetokea jioni ya Juni 24 mwaka huu, kwenye Kijiji cha Mushoji, Kitongoji cha Bishaka, Tarafa ya Bugabo, wilayani Bukoba.

Alisema siku ya tukio, mwanafunzi huyo ambaye alikuwa akiishi na bibi yake Bi. Meriselina Bigira (53), alipeleka chakula kwa mchungaji wao Peter Mabara (25), anayeishi eneo la Machugani.

Aliongeza kuwa, siku hiyo mwanafunzi huyo hakurudi nyumbani kwao kama ilivyokuwa kawaida yake ambapo bibi yake alipata wasiwasi na kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kishanje.

Taarifa hiyo ilitolewa Juni 25 mwaka huu, ambapo baada ya kutafutwa, mwili wake ulikutwa kwenye korongo lililopo katika mbunga ya kuchungia mifugo.

“Mwili wa mwanafunzi huyu ulikuwa umetumbukizwa katika shimbo kichwa chini miguu juu na jiwe kubwa likiwa limemkandamiza kichwani.

“Baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi na daktari, ilibainika alikuwa amevunjwa taya katika shavu la upande wa kulia, shingo pamoja na kubakwa,” alisema Kamanda Kalangi.

Alisema katika uchunguzi huo, walibaini mwili huo ulikuwa na michubuko iliyokuwa ikitoa damu sehemu za siri na nguo za ndani alizokuwa amevaa zilionekana eneo la tukio zikiwa zimechanwa.

Hata hivyo, habari zaidi zinasema chanzo cha mauaji hayo ni Mchungaji Mabara ambaye hivi sasa anashikiliwa na polisi.

Mchungaji huyo alikamatwa jana kwenye Kituo cha Mabasi Bukoba Mjini waakati akitoroka kwenda nyumbani kwao Mjini Kahama, mkoani Shinyanga.

Hivi sasa anashikiliwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa kwa mahojiano zaidi na atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika.

No comments:

Post a Comment