28 June 2012

Mramba, Yona wana kesi ya kujibu



Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema washtakiwa wa kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 11.7, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Basil Mramba, wana kesi ya kujibu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni ambao wote walikuwa Mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Uchumi, Bw. Agrey Mgonja.

Mmoja kati ya mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo, Bw. Sam Lumanyika, aliieleza mahakama kuwa jopo limeona upande wa mashtaka katika kesi hiyo umeweza kuthibitisha tuhuma zinazowakabili washtakiwa bila kuacha shaka.

Kutokana na hali hiyo, mahakama hiyo imepanga washtakiwa hao kuanza kujitetea kuanzia Agosti 22 hadi 24 mwaka huu. Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 12 pamoja na  vithibitisho 17  katika kuthibitisha mashtaka hayo.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Agosti 2002 na Juni 14 2004, jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya fedha hizo.

Ilidaiwa kuwa, washtakiwa hao waliipatia msamaha wa kodi kinyume cha sheria kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza.

No comments:

Post a Comment