28 June 2012

Viongozi wamejiuzia kiwanda cha korosho Mtwara –Mbunge




Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalumu Bi. Christowaja Mtinda (CHADEMA), amesema baadhi ya viongozi serikalini, wamejiuzuia kiwanda cha kubangua Korosho cha Newala One, kilichopo mkoani Mtwara kwa sh. milioni 75 bei ambayo ni sawa na bure na kukigeuza kiwanda hicho kuwa ghala la kuhifadhia korosho.

Alisema mkakati huo ulisukwa kwa makusudi na baadhi ya viongozi wa Serikali ambao walihusika kuuza viwanda vya korosho hivyo kulihujumu zao hilo na kuikosesha Serikali mapato yaliyokuwa yakitokana na viwanda hivyo.

Bi. Mtinda alikuwa akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kusisitiza kuwa, kitendo hicho ni kudidimiza nchi hivyo aliitaka Serikali ieleze hatua watakazochukua kwa viongozi hao.

Alisema asilimia 75 ya viwanda hasa vya korosho, vimebinafsishwa kwa watu walioshindwa kuviendeleza na kuvigeuza maghala ya kuhifadhia zao hilo hasa katika mfumo wa stakabadhi ghalani na kusababisha vife hivyo wananchi wengi kukosa ajira.

“Walionunua kiwanda hiki ni viongozi wa Serikali ambao wamo humu bungeni, huu ni wizi wa wazi kabisa naomba Serikali itoe majibu ya hatua watakazochukua,” alisema Bi. Mtinda.

Hata hivyo, akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Kondoa Kusini, Bw. Juma Nkamia (CCM), aliitaka Serikali kulifuatilia kwa umakini zao la alizeti Kutokana na hujuma wanazofanyiwa wakulima kwani kuna viwanda viwili tu ambavyo ndivyo vinanunua alizeti na kusisitiza kuwa, baadhi ya wabunge wametumwa na wafanyabiashara hao ili kujenga hoja ya viwanda hivyo kuondolewa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

“Hakuna sababu ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje wakati wananchi wa mikoa ya Singida na Dodoma ni wakulima wazuri wa alizeti hivyo ni vyema kuwepo utaratibu mzuri wa kuwanufaisha,” alisema Bw. Nkamia.

Kauli ya Bw. Nkamia kudai kuna wabunge wanaoshawishi kuondolewa VAT katika viwanda hivyo, ilimfanya Mbunge wa Kasulu Mjini, Bw. Moses Machali (NCCR-Mageuzi), kuomba mwongozo wa Spika na kutaka wabunge hao watajwe majina kwani muda mrefu nchi inakabiliwa na kashfa za ufisadi.


No comments:

Post a Comment