Na Mwandishi Wetu, Handeni
SERIKALI imetoa onyo kali kwa Kampuni ya Ujenzi ya Ms Sinohydro ya China na kuitaka kurejesha mitambo iliyohamishwa kwenye mradi wa ujenzi wa Barabara ya Handeni hadi Mkata, inayojengwa kwa kusuasua.
Pia kampuni hiyo imetakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya Handeni hadi Korogwe, mkoani Tanga ambayo ujenzi wake unafanyika kwa kasi ndogo, tofauti na malengo yaliyokusudiwa na serikali.
Onyo hilo lilitolewa eneo la miradi hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. John Ndunguru, alipofanya ziara ya kushitukiza kwenye miradi ya ujenzi wa barabara za Handeni hadi Mkata na ile ya Handeni hadi Korogwe juzi.
Baada ya kutembelea eneo la miradi hiyo, Dkt. Ndunguru alibaini kuwa mkandarasi anayejenga barabara hizo, amehamisha baadhi ya mitambo yake kinyemela na kuipelekwa sehemu zingine, kabla ya kumaliza mradi husika.
Dkt. Ndunguru aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Ms Sinohydro ya China imeshindwa kukamilisha mradi wa kwanza wa ujenzi wa barabara ya Handeni, Mkata yenye urefu wa kilomita 54, kwa wakati, kama ambavyo mkataba unavyoonesha kuwa mradi huo ungeisha mwezi Novemba mwaka jana.
"Mkandarasi anayejenga barabara ya Handeni, Mkata alipaswa kuikabidhi Novemba mwaka jana, hadi sasa anaendelea na ujenzi kwa kusuasua, mbaya zaidi amehamisha baadhi ya mitambo kutoka eneo la mradi, hivyo nimeongea naye, nimemwambia baada ya siku saba, awe amerejesha mitambo hiyo na akabidhi barabara haraka iwezekanavyo", alisema Dkt. Ndunguru.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Handeni, Korogwe yenye urefu wa kilomita 68, Dkt. Ndunguru alisema, pia unajengwa kwa kusuasua, kiasi kwamba mkandarasi huyo akifanyiwa mzaha, atachukuwa muda mrefu kuimaliza.
Haya ni matokeo ya kumpa mtu mmoja kazi nyingi kwa wakati mmoja. Inatakiwa mkandarasi kutokupewa kazi ya pili mpaka amalize aliyonayo na kabla ya kupewa nyingine iangaliwe ya kwanza ameifanya vipi. Ikumbukwe wakandarasi wako wengi hivyo sio vizuri kulimbikiza kazi kwa mtu mmoja wakati wengine hawana kazi yote kwa ajili ya rushwa.
ReplyDelete