02 March 2012

Kauli ya JK urais 2015 yazua mtafaruku

* Yadaiwa inawazibia wenye uwezo, kusababisha mpasuko CCM
Na Reuben Kagaruki
Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya gazeti moja la kila siku (sio Majira) kumnukuu Rais Jakaya Kikwete, akihadharisha watu wa umri wake kuachana na ndoto za urais mwaka 2015, kauli hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na kuzua mtafaruku mkubwa miongoni mwa wanachama na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akifungua Kikao cha Kamati Kuu (CC), jijini Dar es Salaam na kusema kuwa, muda wake wa uongozi ukiisha, angependa nafasi hiyo ishikwe na vijana.

Chanzo chetu kinasema kuwa, Rais Kikwete alisema watu wenye umri kama wake ambao wanataka urais, si wakati wao bali wa vijana kauli ambayo inadaiwa kuwanyong'onyeza baadhi ya makada wanaotajwa kutaka nafasi hiyo wakati umri wao umeenda.

Rais Kikwete ametoa kauli hiyo wakati makundi mbalimbali ndani ya chama hicho, yakijipanga kwa ajili ya kusaka nafasi katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa makada wa chama hicho ambaye pia ni mjumbe wa CC, alidai kusikitishwa na kauli hiyo na kuhoji mantiki ya kuwabagua watu wenye umri kama wake katika nafasi hiyo ya juu.

Kada huyo ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe, alisema haoni sababu ya Rais Kikwete kuwakatisha tama viongozi wa umri wake bila kuzingatia kigezo cha uwezo na sifa zao.

Alisema kimantiki, hata yeye Rais Kikwete kwa umri atakaostaafu mwaka 2015, hatakuwa mzee na asingechaguliwa mwaka 2005, bado alikuwa na nguvu na uwezo wa kuwania nafasi hiyo pia asingejisikia vizuri kama angesikia kauli hiyo.

Aliongeza kuwa, urais si kazi ya umri, kinachoangaliwa ni uwezo ambapo kauli ya Rais Kikwete, imeongeza mpasuko ndani ya chama hicho katika kinyang’anyoro cha urais na kama CCM haitakuwa makini, unaweza kutokea mgawanyiko mkubwa.

“Karibu asilimia 100 ya watu wanaohusishwa na urais 2015 wana umri kama wa rais, hawa si watu wa hivi hivi tu, wana uwezo na rekodi kubwa kiuongozi ndani na nje ya chama.

“Umri wao utakapotumika kama kigezo cha kuwahukumu wasipate nafasi hiyo, Rais ambaye ni Mwenyekiti wa chama chetu anakosea,” alidai kada huyo ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini. 

Kada mwingine wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, alidai kusikitishwa na kauli hiyo kwa madai kuwa, inakigawa chama na kudhoofisha mshikamo uliopo.

“Hii kauli inanipa hofu, kumbuka wale wenye umri kama wake wako wengi na wengine waligombea naye, sasa wakiamua waungane wawe kundi moja, waanzishe mtandao wao itakuwa ni hatari kwa chama chetu, kauli hii inaweza kufifisha chama na kukiweka pabaya kwa kuleta mgawanyiko,” alisema kada huyo.
   
Akithibitisha kuwa urais si suala la umri, aliwataja baadhi ya viongozi wa nchi za  Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe , Uganda, Sudani na zingine za Afrika kuwa zinaongozwa na watu wenye umri wa kutosha kabisa.

Aliwataka wana CCM kujenga mshikamano zaidi na kutoruhusu mitazamo ya kuleta mgawanyiko ndani ya chama hicho.

“Kama CCM itafanya mchezo huu, ikumbuke kuwa wapo wenzetu wanaotazama mtu kwa uwezo wake na si kwa umri kama CHADEMA, watatuadhiri hivi hivi, tuache mchezo,” alionya kada huyo.



  



 



7 comments:

  1. Kikwete siyo kiongozi makini nafikiri ni Kiwete wa akili,hivi umri na uongozi wa nchi vina tija gani?.Kwani yeye alipogombea Uraisi hakuwa mzee sasa anatufanyia nini WaTZ kama siyo ubabaishaji na usanii tu?.Mie namuona kama angeanza kuwa msanii na kutunga nyimbo kusaidiana na Kapteni Komba wa TOT maana inakufa .He is the non serious President at all.We messed up and won't do again.Afterall he isn't mandated to make choice for Tanzanians may be ,he will influence the president for his own family.

    ReplyDelete
  2. Kwa kweli mheshimiwa Rais kikwete amekosea kutumia busara kwa jambo hili.japokuwa sijajua kama ni maoni yake binafsi au imeshakuwa sheria.ningependa apendekeze umri wa kugombea kiti cha uraisi uwe kuanzia umri wa miaka 35 na kuendelea.
    katika umri wake kuna watu wenye uwezo wa kuchapa kazi vizuri sana tena kukupita weye mheshimiwa raisi.haina haja ya kuandikia mate.kwa mfano mheshiwa john pombe magufuri ni kiongozi mchapa kazi mzuri.nafikilia hutoba uliyotuhubia umeikosea kuisoma.

    ReplyDelete
  3. TUKIANZA KUANGALIA UMRI BASI WENYE SIFA NZURI TUTAWAWEKA KANDO NA KUJIKUTA TUNAMCHAGUA MSANII KAMA YEYE .MCHEZA NGOMA NI MCHEZA NGOMA TU HANA JIPYA

    ReplyDelete
  4. Kikwete ameonyesha udhaifu katika uongozi wake ambao wengi hatukuutegemea kuuona kabisa. Sasa anataka pia atuchagulie kiongozi wa aina yake? Hapana, hili waTanzania walikatae kwa nguvu zote.

    Huyu bwana sijui waTanzania walimchagua kwa vigezo gani, maana ameonyesha kushindwa kabisa katika nyanja zote! Hata kufikiri kwake ni kwa wasiwasi tupu! Kama anataka kuisambaratisha CCM, amekwishafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, sasa anataka kuiua kabisa. Historia itamshitaki hivyo.

    ReplyDelete
  5. Huyu Rais ana vituko. Kama ni hili la urais na uzee,baadae atakuja kutuambia na sisi wazee tusioe wala kina mama wa umri wasiolewe. Atoe sababu za kimsingi!

    ReplyDelete
  6. watanzania tusipoteze ustaarabu wetu,hakuna sababu ya kumkejeli Rais wa nchi kwa kutoa maoni yake.Yeye ni binadamu sawa na wewe na mimi.Alichosema Mhe.Rais ndiyo kanuni ya maumbile kwamba kitu chochote kipya au kichanga ni bora kuliko kizee au kikukuu mfano binadamu,gari shamba,nyumba n.k kadiri vinavyotumika vinachakaa.Tatizo letu hatutaki ukweli au kufahamu uyakinifu wa kisayansi.Hakuna kosa lolote katika kauli ya Rais ndiyo ukweli wenyewe.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kama kuna ukweli katika kauli ya Kikwete, ukweli huo ni kwamba hao wenye rika lake wanaotafuta urais baada ya ngwe yake hii ni udhaifu wao ulioruhusu mtu dhaifu kama huyu kuchukua uongozi wa nchi hii miaka kumi. Ni sifa hiyo pekee ya kutokuwa na ujasiri wa kusimama na kumpinga ndio inayoweza kuwanyima kupewa uongozi baada ya ngwe yake kuisha hapo 2015.

      Delete