20 March 2012

Wapinzani wa Simba kutua kesho

Na Zahoro Mlanzi
WAPINZANI wa Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho timu ya ES Setif ya Algeria, inatarajia kutua nchini kesho na msafara wa watu 35 kwa ajili ya mechi yao itakayopigwa Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kwa mujibu wa taarifa walizopata kutoka kwa Chama cha Soka cha nchini humo, zilieleza kwamba timu hiyo itatua saa 11.45 alfajiri ya siku hiyo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri.

Alisema kwa sasa wanafanya mawasiliano na ubalozi wao nchini, juu ya kupata viza kwani wanataka mpaka watakapotua wawe tayari wameshawakatia.

"Katika msafara huo utahusisha wachezaji, waandishi wa habari na viongozi wa FA (Chama cha soka) na benchi lao la ufundi, ambapo taratibu zingine wapi watafikia hilo wanalifanyia kazi wenyeji wao Simba," alisema Wambura.

Alisema timu yao inaundwa na wachezaji wazawa ila kocha mkuu wao, Alain Gaiger ni raia wa Uswisi na wana imani Simba itakamilisha kila kitu kwa wakati muafaka.

Akizungumzia suala la waamuzi watakaochezesha mechi siku ya kuja, alisema hilo wenyeji wao, Simba wanajua lini wanapaswa kuja na hoteli watakayofikia.

Waamuzi hao ni Hudu Munyemana ambaye atakuwa kati na wasaidizi wake Felicien Kabanda, Theodgene Ndagijimana na Edouard Bahizi wote kutoka Rwanda.

Kuhusu kujipanga juu ya vurugu zilizojitokeza hivi karibu kwenye Uwanja wa Taifa, Wambura alisema kikubwa mashabiki wenyewe wanapaswa kujua namna wanavyotakiwa kushangilia na pia elimu zitaendelea kutolewa.

Alisema vurugu zisizo za maana zinaweza kuiweka Simba katika wakati mgumu kwa CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika), kuiondoa mashindanoni na pia watashirikiana na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuhakikisha usalama unakuwepo wa kutosha.

Simba ilifuzu hatua hiyo kwa kuiondosha Kiyovu ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2 ambapo katika mechi ya kwanza iliyopigwa Kigali, zilitoka sare ya bao 1-1 na marudiano ikashinda 2-1.





No comments:

Post a Comment