16 March 2012

RC aagiza watendaji kusimamia mazingira

Grace Ndossa na Florah Temba, Kilimanjaro
WATENDAJI wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kusimamia sheria za mazingira zilizopo na kuhakikisha wanapiga marufuku matumizi ya mbao katika kutengeneza samani na ujenzi ili kuhakikisha mazingira yanarudi katika hali yake ya awali.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Leonidas Gama wakati akizungumza na watendaji wa halmashauri hiyo ikiwa ni moja ya mipango yake ya kutembelea halmashauri za mkoa huo na kuangalia mpango mkakati wa halmashauri wa kulinda na kutunza mazingira.

Bw.Gama alisema, kwa sasa mkoa umesitisha matumizi ya mbao kutokana na kuonekana kukatwa kwa miti ya asili kinyume cha sheria hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa inachangia uharibifu wa mazingira.

Alisema, ili kuhakikisha mpango mkakati wa kulinda na kuhifadhi mazingira unafanikiwa ni vema watendaji wakasimamia sheria na kuhakikisha zinatekelezwa ipasavyo na asiwepo mtu ambaye atakiuka sheria kwa maslahi binafsi na kuyahujumu mazingira jambo ambalo alisema linaleta madhara kwa mkoa mzima wa Kilimanjaro.

Awali akisoma mpango mkakati wa Manispaa ya Moshi Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bi. Bernadette Kinabo alikiri kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira na misitu inayozinguka Mlima Kilimanjaro hali ambayo imesababisha kupungua kwa theluji katika mlima huo ikiwa ni pamoja na kupungua kwa maji katika vyanzo vya maji.

Bi. Kinabo alisema, kutokana na uharibifu huo halmashauri hiyo imeweka mikakati mbalimbali ya upandaji miti ili kuweza kunusuru hali hiyo na hatimaye kuwa na uwezo wa kupambana na hali ya tabia nchi ambapo matokeo yake yanatarajiwa kuwezesha Moshi kuwa na hali nzuri ya kimazingira.

Alisema, moja ya mikakati hiyo ni upandaji wa miti 1,680,000 kwa kila mwaka kwa wakazi 210,000 wa manispaa hiyo ambapo kila mkazi anatakiwa kupanda miti nane kwa mwaka na kwamba mkakati huo utatekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira.

Alisema, mkakati mwingine ni kuwa na kampeni ya upandaji aina ya miti inayokuwa kwa haraka ikiwa ni pamoja na upandaji miti katika maeneo ya shule, makazi ya watu, zahanati, vituo vya afya, barabara, maeneo ya taasisi za kidini, magereza, hifadhi ya mito na makorongo.

Hata hivyo kutokana na kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira uliochangiwa na ukataji miti ovyo katika Mkoa wa Kilimanjaro, mkoa huo umepanga kuendesha kampeni kubwa ya upandaji miti itakayozinduliwa Aprili Mosi, mwaka huu na kwenda hadi Aprili 10, lengo likiwa ni kurudisha hali ya mazingira kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na uoto wa asili katika misitu na maeneo ya vyanzo vya maji.

Wakati huo huo mwandishi wetu kutoka Siha anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw.Leonidas Gama amewataka watendaji kusitisha kutoa vibali vya upasuaji wa mbao katika maeneo yao ili kudhibiti uharibifu wa mazingira pamoja na kuhifadhi uoto wa asili.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa mazingira wilayani Siha hivi karibuni, Bw. Gama alisema ili kudhibiti uharibifu wa mazingira lazima kufunga utoaji wa viabali vya upasuaji na ukataji miti ovyo katika mazingira yanayowazunguka.

Alisema, hiyo ni kauli mbiu ya kuhamasisha upandaji miti ili kuepuka eneo hilo kuwa jangwa kutokana na utafiti uioafanywa na wataalamu kutoa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walibaini kuwa endapo hatua madhubuti za kuhifadhi mazingira katika eneo hilo hazitachukuliwa miaka 20 ijayo kutageuka jangwa.

“Lazima watendaji wa serikali za mitaa na wenyeviti kuhakikisha hakuna vibali vinavyotolewa kwa mtu yoyote ama kukata miti katika eneo lake kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kuhifadhi mazingiara na kuyaweka katika hali nzuri,”alisema Bw. Gama.

Pia alisema, eneo lolote lile ambalo litabainika kuwa na upasuaji wa mbao au kukata miti bila kuwepo kwa taarifa watakao wajibika wa kwanza ni mwenyekiti wa eneo hilo pamoja na ofisa mtendaji wa kata.

Hata hivyo alisema, hakuna kutoa vibali wa kujenga katika eneo lolote hadi hapo mtu anayetaka kujenga kupanda miti nane  katika eneo hilo na ikaguliwe kwanza ndipo ataweza kupatia kibali cha kuendelea na ujenzi.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Aggrey Mwanri alisema, ni lazima hatua kali zichukuliwe ili waweze kunusuru wilaya hiyo na jangwa.

Alisema, watendaji wanatakiwa kuwajibika katika kufanya kazi yake kama alivyochaguliwa na kama hawawezi kazi hiyo aaachie ngazi wengine waendelee na kazi.

“Sipo kwa ajili ya kutishia watu, nachochea maendeleo ya jimboni kwangu, mtendaji wa kijiji ambaye hawezi kuwa na bustani ya miti na kusimamisha sheria hatufai, kwani tunataka viongozi wanaowajibika kutumikia wananchi waliowachagua,”alisema.

No comments:

Post a Comment