Ofisa uhamiaji mkoa wa Shinyanga,Bw. Selemani Kameya (Picha na Suleiman Abeid)
Na Suleiman Abeid
TATIZO la wahamiaji haramu nchini hivi sasa linaelekea kuwa sugu kufuatia matukio ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa makundi ya wahamiaji hao kutoka nchi za Somalia na Ethiopia zilizopo katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.
Mwishoni mwa mwaka 2011 zaidi ya wahabeshi 103 walikamatwa kwa kosa la kuingia nchini bila hati za kusafiria wala vibali kutoka mamlaka husika ya serikali, pia Januari mwaka huu wahamiaji wengine 98 wanaodaiwa kuwa raia wa Somalia walikamatwa mkoani Morogoro.
Huu ni mfano tu wa tatizo la makundi ya wahamiaji haramu kuingia nchini kinyume cha sheria ambapo baadhi yao huwa ni wapitaji wanaokwenda nchini Afrika Kusini kutafuta hifadhi kama wakimbizi.
Hata hivyo baadhi ya wahamiaji hao hubaki nchini kwa kujichanganya na raia wengine hali ambayo huwawezesha kufanya shughuli mbalimbali za kijamii pasipo kubainika kwamba wao si raia.
Pamoja na kwamba Afrika ni moja na wananchi wake ni ndugu, lakini baadhi ya ndugu zetu hawa wanaoingia nchini huwa na malengo tofauti ambapo hujiingiza katika vitendo vya kufanya uhalifu ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha.
Baadhi ya matukio mengi ya unyang’anyi wa kutumia silaha yaliyokwisharipotiwa mkoani Shinyanga wahusika wake huwa ni wahamiaji haramu kutoka nchi jirani hasa wale wa kutoka nchi za Rwanda na Burundi ambao huingia nchini kama wakimbizi wanaokimbia vita katika nchi zao.
Vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha mara nyingi vimesababisha ndugu zetu wasio na hatia kupoteza maisha na kupoteza mali zao ambapo kwa wafanyabiashara hujikuta wanapoteza mitaji yao baada ya kunyang’anywa mali zao katika matukio mbalimbali ya utekaji wa magari.
Matukio ya utekaji magari ya abiria mara nyingi yameripotiwa kutokea wilayani Kahama na Bukombe, mkoani Shinyanga mapori ya Biharamulo na Nyakanazi mkoani Kagera na maeneo ya mapori yaliyoko katika barabara ya kutoka mkoa wa Kigoma.
Asilimia kubwa ya watuhumiwa wanaokamatwa kutokana na kuhusika na matukio hayo huwa sio watanzania hali ambayo inaonesha wazi tatizo la nchi inapotokea kuvamiwa kwa wingi na wimbi la wahamiaji haramu.
Kutokana na hali hiyo serikali kupitia idara yake ya uhamiaji imekuwa ikifanya kila juhudi ili kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu ambapo pia idara hiyo imekuwa ikitoa wito kwa raia wema kutoa taarifa kwa maofisa wa uhamiaji pale wanapobaini kuwepo kwa watu wanaowatilia shaka kuwa si watanzania.
Pamoja na juhudi hizo lakini bado tatizo hilo limeendelea kusumbua ambapo hazipiti siku bila kusikia taarifa za kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Hata hivyo imebainika kuwa baadhi ya wahamiaji hao wamekuwa wakifanikiwa kuingia nchini kutokana na msaada wanaopewa na watanzania wenzetu baada ya kupewa kitu kidogo ambacho huridhika nacho na kusahau madhara ambayo wahamiaji hao wanaweza kuwasababishia.
Katika kukabiliana na hali hiyo, idara ya uhamiaji mkoani Shinyanga, imebuni mpango mpya wa kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu utaratibu ambao inaaminika ukitumika vizuri utasaidia kupunguza tatizo.
Mpango huo ni “Uhamiaji Shirikishi” mpango ambao umebuniwa kutoka katika mpango ulioanzishwa na Jeshi la Polisi nchini wa “Ulinzi Shirikishi” ikitarajiwa kwamba utasaidia kukabiliana na matukio ya uhalifu katika maeneo mengi nchini.
Ofisa Uhamiaji wa mkoa, Bw. Selemani Kameya anasema mpango wa “Uhamiaji Shirikishi” umebuniwa ili kuwawezesha raia wengine kuisaidia idara yake katika kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu.
Bw. Kameya anasema, “Ilivyo Polisi Jamii, idara imeanzisha mpango wa Uhamiaji Shirikishi, lengo likiwa ni kupata taarifa mbalimbali za wahamiaji haramu kutoka kwa raia, pia kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya wahamiaji haramu,”
“Tatizo la wahamiaji haramu halileti madhara kwa serikali peke yake, hata wananchi wetu wanaathirika kutokana na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na wahamiaji hao, kutokana na hali hiyo tumeona ni vyema wananchi nao wakashiriki katika kukabiliana nao.”
Katika kipindi cha mwaka huu wa 2012, idara ya uhamiaji mkoani Shinyanga imejiwekea mikakati kadhaa katika mapambano dhidi ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini kupitia njia za panya.
Bw. Kameya anasema, moja ya mikakati hiyo ni kuzidisha juhudi katika kuelimisha wananchi wa mkoa wa Shinyanga juu ya dhana nzima ya wahamiaji haramu na madhara yake.
“Aidha tutazidisha kazi kubwa ya udhibiti wa wahamiaji hao haramu, ambapo tunatoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga kutoa ushirikiano kwa idara yetu katika kutekeleza wajibu wake na kuacha kujihusisha na vitendo vya kushirikiana au kusaidiana na wahamiaji haramu,”
“Mkakati mwingine tuliojipangia mwaka huu ni kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika sehemu zote zenye mikusanyiko, migodini, viwandani, makazi ya watu, nyumba za kulala wageni na sehemu nyingine hii itakwenda sambamba na kuendeleza mpango huo ,” anasema Bw. Kameya.
Anasema, pamoja na mikakati waliyojiwekea, lakini bado kuna changamoto zinazowakabili, ikiwemo wananchi wengi kutoelewa madhara ya kuwahifadhi na kushirikiana na wahamiaji haramu ambapo wengine hudiriki kuwaajiri katika maeneo yao ya kazi.
Changamoto nyingine ni uchache wa wafanyakazi katika idara hiyo, ukosefu wa vitendea kazi vya kutosha kama vile magari kwa ajili ya kurahisisha usafiri wa kwenda katika maeneo mbalimbali kuendesha misako dhidi ya wahamiaji haramu.
Bw. Kameya anasema, katika kipindi cha mwaka 2011 idara yake ilifanikiwa kukusanya maduhuli ya serikali sh 140,200,000 na dola za Marekani 343,200 ikilinganishwa na sh 114,870,000 na dola za Marekani 142,780 zilizokusanywa mwaka 2010.
Anasema wahamiaji haramu waliokamatwa mwaka 2011 walikuwa 255 ikilinganishwa na watu 119 waliokamatwa mwaka 2010 ambapo katika kipindi cha mwaka jana idara hiyo iliweza kukamata watanzania 98 waliotuhumiwa kwa kosa la kuwahifadhi kinyume cha sheria wahamiaji haramu.
No comments:
Post a Comment