02 March 2012

Abiria Mv Maendeleo wanusurika kufa maji

Na Reuben Kagaruki
ABIRIA 450 waliosafiri na Meli ya Mv Maendeleo kutoka Unguja kwenda Pemba, jana walikumbwa na hofu kubwa ya kufa maji baada ya meli hiyo kupotea njia na kugota kwenye kina kidogo cha maji.

Wakizungumza na Majira kutoka eneo la tukio, baadhi ya abiria waliosafiri na meli hiyo walisema walikwama kuanzia saa 11 alfajiri wakiwa umbali wa kilometa 180, karibu na bandari ya Pemba.

Kwa mujibu mtoa taarifa, hali hiyo ilijitokeza baada ya boya lililowekwa baharini kwa ajili ya kumpa maelekezo nahodha, kusukumwa na maji hivyo alilifuat na kujikuta meli yake ikikwama.

Meli hiyo ilitarajiwa kutia nanga kwenye bandari ya Pemba saa 12 asubuhi jana, lakini ilikuwa hadi jioni ilikuwa hajaondolewa. Hata hivyo abiria walifanikiwa kuhamishwa kwa boti.

“Kwa kweli hali ilikuwa mbaya, tulikaa eneo la tukio kwa zaidi ya saa sita, tukio hili lilitukumbusha mengi hasa lile la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders,” alisema abiria aliyesafiri na meli hiyo kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini.

Alisema baada ya mtafaruku huo, baadaye hatua za kuokoa abiria zilizochukuliwa huku meli hiyo ikiwa tayari imefungwa kamba kuizuia isiendelee kupelekwa mbali zaidi na maji wakati jitihada za kutafuta boti kwa ajili ya kuhamisha abiria kutoka kwenye meli hiyo  zikiendelea.

Mtoa habari huyo ambaye alikuwa akienda kisiwani Pemba kuhudhuria harusi ya ndugu yake, alisema “Watu walikuwa na hofu kubwa huku wengine wakitamani kuanza kuvaa maboya tayari kwa kujiokoa endapo hali ya hatari ingetokea," alisema.

Mwaka 2011, meli ya MV Spice Islanders ikitoka Unguja kwenda Pemba, ilizama eneo la Nungwi na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200 huku wengine 250 wakiokolewa.

Tangu kuzama kwa meli hiyo na nyingine iliyotanguliwa ya Mv Bukoba mwaka 1996 na kusababisha vifo vya watu zaidi 800, watu wengi wamekuwa wakikumbwa na hofu kubwa pale vyombo vya maji vinapopata hitilafu majini.

No comments:

Post a Comment