27 February 2012

Ajali yaua watano, yajeruhi 11 Mbeya

*Polisi wabaini uhalifu mpya unaofanywa na walemavu

Rashid Mkwinda, Mbozi
na Moses Mabula, Igunga

WATU watano wamefariki dunia na wengine 11 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la abiria aina ya Coster namba T. 173 ATS linalofanya safari kati ya Mbeya na Tunduma.

Gari hiyo iligongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lenye namba za usajili  T. 847 AKS, ambalo lilikuwa likienda Tunduma.

Katika ajali hiyo, watu wanne walikufa papo hapo na mmoja alifariki wakati akikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Mjini Vwawa wilayani Mbozi.

Mashuhuda wa ajali hiyo walisema ilitokea saa nane mchana ambapo lori aina ya Fuso lililokuwa likitokea barabara ya Mbeya, lilipoteza mwelekeo na kuliparamia basi hilo upande wa kulia na  kusababisha vifo na majeruhi.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Charles Mkombachepa, alisema alipokea maiti tano na majeruhi 11.

Alisema marehemu waliotambuliwa katika ajali hiyo ni Bi. Tabu Msongole(35) aliyekuwa na mwanaye wa mwaka mmoja na nusu aliyetambuliwa ka jina la Aron Mwashela ambapo miili ya watu watatu bado haijatambuliwa.

Aliwataja majeruhi kuwa ni Bw. Mbaraka Ally (45) Bw. Kenethy Mwampashe, Bw. Ngwele Charles, Bi. Christina Mwawalo (40), Bi. Aida Mwasenga (29), Bw. Luka Nzunda(32) na Bw. Immanuel Simbeye (18).

Aliongeza kuwa, kati ya majeruhi waliolazwa watatu wamepata majeraha ya kichwani na watakuwa chini ya uangalizi maalumu pamoja na kupigwa picha za mionzi ili kubaini matatizo zaidi.

Dkt. Mkombacheka alisema majeruhi mmoja Bw. Kenedy Mwampashe ambaye amevunjika mfupa wa paja, atahamishiwa   Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa ajili ya matibabu zaidi wakati majeruhi wengine watatu, wataendelea kuwa chini ya uangalizi wa
madaktari wa kawaida.

Jeshi la Polis limethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo uchunguzi unafanywa kujua chanzo chake.

Wakati huo huo watu wawili wamefariki dunia katika Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, kwa kupigwa na radi wakati mvua ikinyesha.

Akizungunmza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Antony Rutta, alisema tukio hilo limetokea Februari 24 mwaka huu saa mbili usiku katika Kijiji cha Kuramawe, Kata ya Nguvu Mmoja.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Bw. Juma Hingo (24) na Tango Hingo (26) wote wa familia moja ambaop walipigwa na radi wakati wakirejea nyumbani kwao wakitoka katika matembezi.

Mwandishi wetu Masau Bwire, anaripoti kutoka Kibaha kuwa, Jeshi la Polisi mkoani Pwani, limebaini mbinu mpya wanayoitumia wahalifu ili kukwepa mkono wa dola kwa kuwatumia watu wenye ulemavu kufanikisha uhalifu wao.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Salehe Mbaga, imesema jeshi hilo limebaini mbinu hiyo baada ya kuwakamata watu watatu akiwemo mlemavu wa ngozi (albino) wakiwa na kete 10 za dawa za kulevya aina ya heroin pamoja na sigara ambayo waliitoa tumbaku na kujaza dawa hiyo.

Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Kamanda Mbaga, Ofisa Habari wa jeshi hilo mkoani hapa, Bw. Athmani Mtasha, alisema watu hao walikamatwa Februari 25 mwaka huu, saa saba usiku kwenye Kijiji cha Kwa Mfipa na kukiri kutumika katika biashara hiyo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bw. Juma Mwalimu (35), mkazi wa Kwa Mfipa, Bw. Ally Ramadhani (29), mkazi wa Maili Moja na Bw. John Lameck (20), kwa jina maarufu 'Uliza', ambaye ni albino aliyekodiwa kwa kazi hiyo kutoka Kimara, Dar es salaam.

“Katika mazingira ya kawaida ni vigumu kumpekua mlemavu wa ngozi, viungo au kumuhusisha na uhalifu lakini kuanzia sasa, tutalazimika kuwapekua kama watatiliwa shaka,” alisema.

Alisema watuhumiwa hao bado wanahojiwa na katika Kituo cha Polisi Tumbi na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Kamanda Mbaga alitoa mwito kwa watu wenye ulemavu kutokubali katika katika matukio ya uhalifu kwa tamaa za watu wachache na kujiingiza kwenye matatizo na  hatimaye kifungwa gerezani.


No comments:

Post a Comment