23 February 2012

Wazazi Zanzibar washauriwa kuwalea watoto kimaadi

Na Mwandishi Maalumu, Ikulu Zanzibar
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein akiwapungia mkono wananchi waliofika kumpokea wakati alipowasili jana katika Bandari ya Kisiwa cha Tumbatu, ampapo aliudhuria katika sherehe za uzinduzi wa Maulidi ya kuzaliwa Nabii Muhammad (S.A.W), yaliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Tumbatu Gomani. (Picha na Ikulu Zanzibar)


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amewataka walezi na wazazi nchini kuwalea watoto wao kwa kufuata utamaduni na maadili ya Kiislamu na mwendendo wa Mtume Muhammad (S.A.W) ili waweze kuishi maisha bora yenye amani na upendo.

Mwito huo aliutoa jana mjini Tumbatu Gomani katika uzinduzi wa Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad ambayo ilifanyikia Msikiti Mkuu wa Ijumaa Gomani na kuudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama, dini na Serikali kutoka ndani na nje wakiwemo wananchi.

Akitoa nasaha zake kwa wananchi walioudhuria katika Maulid hiyo, Dkt.Shein alisema iwapo wazazi na walezi watachukua jukumu hilo la kuwalea watoto kwa kufuata misingi ya Kiislamu kama ilivyoelezwa katika Qur-an Tukufu na hadithi za Mtume Muhamad, watoto watakuwa na maadili yanayozingatia malezi mazuri.

Alisema, ni jukumu la wazazi kuwalea watoto katika mafundisho ya Kiislamu ili nao wawe na maadili bora na kujenga maisha yanayoendana na ushindani.

Dkt.Shein alisema, Serikali yake kwa upande wake imekuwa ikichukua juhudi katika kuhakikisha watoto wanapata elimu ambayo itaweza kuwasaidia katika maisha yao ya duniani na 'akhera' ikiwa ni pamoja na kuwajengea misingi bora kuanzia awali hadi vyuo vikuu.

Aliwaeleza wananchi hao wa Tumbatu kuwa pamoja na hayo yote pia, Waislamu wanapaswa kutambua mbali na mambo mengine jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanamcha Mungu wakati wowote.

Awali Mufti Mkuu wa Zanzibar wakati akimkaribisha, Dkt.Shein alieleza juu ya historia fupi ya kuingia kwa dini ya Kiislamu Zanzibar huku akieleza sifa za misingi ya Mtume Muhammad ambapo alisisitiza ni vyema utaratibu huo ukafuatwa kwa kuzingatia misingi ya imani.

Sheikh Othman Maalim alisema, kuna kila sababu ya Waislamu kukaa pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumsifu Mtume Muhammad bila kuchoka.

Hata hivyo mamia ya wananchi wa Tumbatu pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo mwenyeji mkuu wa shughuli hiyo, Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala, Bw. Alhaj Haji Omar Kheir walimpokea, Rais Shein katika Bandari ya Kichangani.

Baada ya kumaliza shughuli hiyo walimsindikiza kuelekea Bandari ya Jendweni kwa safari ya kurudi nyumbani yeye na ujumbe wake pamoja na viongozi, mashekhe na wananchi wengine waalikwa.

No comments:

Post a Comment