23 February 2012

Yanga, Zamalek kama kawa Cairo

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema mpaka sasa hakuna mabadiliko yoyote ya mechi ya marudiano kati ya mabingwa wa Ligi Kuu, Bara na Zamalek ya Misri, hivyo mechi hiyo itapigwa jijini Cairo nchini humo kama ilivyopangwa awali.

TFF ilitoa ufafanuzi huo, baada ya vyombo mbalimbali vya habari nchini kuripoti habari kuwa mechi hiyo, huenda ikachezwa Sudan au Algeria kutokana na vurugu za mashabiki wa soka nchini Misri zilizosababisha zaidi ya watu 74 kupoteza maisha.

Vurugu hizo zilitokea katika mji wa Port Said wakati timu ya Al-Masry ilipokuwa ikiongoza kwa mabao 3-1 dhidi ya Al-Ahly, ushindi ambao umeelezwa kuwa ni wa kihistoria kwa timu hiyo dhidi ya wapinzani wao katika mechi za Ligi Kuu nchini Misri.

Akijibu swali hilo juu ya hatima ya mechi hiyo Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura alisema kama kungekuwa na mabadiliko yoyote ni lazima CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika), ingesema mapema.

"Tunachojua mpaka hivi sasa kama shirikisho, ni kwamba mechi hiyo itapigwa Cairo ila kama kutakuwa na mabadiliko yoyote tutatoa taarifa, mabadiliko yakiwemo basi ni lazima vyama vya nchi husika na waamuzi wangejulishwa mapema," alisema Wambura.

Alisema CAF hawawezi kufanya mabadiliko bila kuwahusisha wadau wao, kwani kuna mambo yanatakiwa yafanyike na si suala la kubadili kirahisi kama watu wanavyodhania.

Yanga mara baada ya kutokea machafuko hayo nchini Misri, iliiandikia CAF barua kuomba mechi ya mkondo mmoja na ikiwezekana ichezwe moja Dar es Salaam tu, lakini CAF iliwajibu ni lazima icheze mechi mbili.

Katika taarifa hiyo ya CAF, ilieleza kwamba endapo wataona kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo, watawajulisha ambapo pia waliiruhusu Ligi Kuu Misri iendelee lakini mechi hazitakuwa na washangiliaji.

Kutokana na hali hiyo, hata mechi ya marudiano kati ya Yanga na Zamalek ambayo inayotarajiwa kuchezwa jijini Cairo haitakuwa na mashabiki zaidi ya waamuzi wa akiba na kamishina wa mchezo.






No comments:

Post a Comment