24 February 2012

Wavuvi kesi ya Magufuli jela miaka 20

Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewakuhumu kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya sh. bilioni 20 washtakiwa wawili kati ya watano katika kesi ya uvuvi wa samaki kwenye Ukanda wa Kiuchumi wa Tanzania (EEZ), bila kuwa na kibali baada ya kupatikana na hatia.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Jaji Agustino Mwarija baada ya kuletwa kwa ajili ya kusomewa hukumu.

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Bw. Hsu Chin Tai (63), ambaye ni Nahodha wa meli waliyokuwa wakiitumia kwa shughuli za uvuvi inayoitwa Tawaliq 1, na Bw. Zhao Hanquing wote raia wa China ambaye alikuwa wakala wa meli hiyo.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mwarija alisema katika shtaka la kwanza la kuvua samaki katika ukanda huo, washtakiwa wote walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya sh. bilioni moja kila mmoja.

Katika kosa la pili la kuchafua mazingira kutokana na uvuvi huo, mshtakiwa Bw. Tai, ndiye alipatikana na hatia ambapo mahakama ilimuhukumu kifungo cha miaka 10 jela au kulipa faini ya sh. bilioni 20 ambapo adhabu hizo zitatumikiwa kwa pamoja.

Wakati huo huo, mahakama hiyo imeamuru meli iliyohusika katika uvuvi huo, itaifishwe kwa sababu ilikuwa haijulikani na Tume inayojihusisha na shughuli za uvuvi katika Bahari ya India (IOCT)

Alisema meli hiyo ilikuwa ikitumia leseni mbili tofauti hali ambayo inaonesha kuwa ilikuwa ikitumiwa katika shughuli za uhalifu hivyo ni sahihi kutaifishwa.

Kuhusu samaki waliokuwa wamekamatwa katika meli hiyo, Jaji Mwarija alisema hakuna amri yoyote itakayotolewa kwa kuwa samaki hao waligaiwa bure kwa taasisi mbalimbali na jamii.

Kwa mujibu wa Jaji Mwarija, adhabu hiyo ni ya kiwango cha chini kisheria kulingana na kosa walilolitenda.

Walioachiwa huru ni Bw. Hsu Sheng Pao ambaye pia akikuwa wakala wa meli hiyo na wahandisi wawili wa meli hiyo Bw. Cai Dong Li na  Bw. Chen Rui Hai.

Washtakiwa hao wameachiwa kutokana na ushahidi ulioletwa mahakamani hapo kutotoshereza kuwatia hatiani.

Awali kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, wakili wa Serikali Bw. Biswalo Muganga, aliitaka mahakama itowe adhabu kali kwa washtakiwa hao kutokana na hasara kubwa walioisababishia Serikali kutokana na uvuvi huo.

Bw. Muganga aliitaka mahakama hiyo itaifishe meli iliyohusika katika uhalifu huo kama kifungu namba 3 (61) cha kanuni ya adhabu kinavyosema.

Wakili wa utetezi Bw. Ibrahim Bendera, aliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu washtakiwa hao kwa kuwa ni kosa lao la kwanza kulifanya nchini na walionesha ushirikiano mzuri tangu walipokamatwa.

Alidai kuwa, washtakiwa hao ni raia wa nchi rafiki na Tanzania na wamekaa mahabusu muda mrefu tangu shauri lao lifikishwe mahakamani.

Alisema mshtakiwa Bw. Tai ni mzee ambaye amekaa gerezani kwa miaka mitatu wakati kesi ikiendelea hivyo miaka hiyo iwe sehemu ya adhabu atakayopewa.

Katika hatua nyingine, aliiomba meli iliyohusika katika uhalifu huo ifanyiwe tathmini ili mmiliki wake alipe fidia au iweze kuuzwa ili Serikali iondokane na gharama ya kuihudumia.

Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na wakili Bw. Bendera na Bw. John Mapinduzi huku upande wa Serikali ukitetewa na wakili Mwandamizi Bw. Muganga  akisaidiana na Bw. Prosper Mwangamila na Bw. Peter Maugo.

Kesi hiyo maarufu kama kesi ya Samaki wa Magufuli, washtakiwa watano wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya shughuli za uvuvi katika wa EEZ bila kuwa na kibali na kuchafua mazingira ya bahari.

Awali kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa 34 ambapo baadhi yao waliachiwa huru kutokana na kuonekana kutokuwa na hatia na kubaki watano hadi jana waliposomewa hukumu.

Mapema Machi 2009, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya kukamatwa wakiwa katika meli ya Tawariq 1 wakifanya uvuvi katika kina kirefu bila leseni ya uvuvi na kuchafua mazingira.

No comments:

Post a Comment