24 February 2012

Mwisho wa matumizi ya analojia EAC Desemba

Na Agnes Mwaijega
SERIKALI kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imevitaka vituo vyote vya utangazaji, vinavyotumia teknolojia ya analojia kuacha kutumia mfumo ifikapo Desemba 31, mwaka huu.

Hatua hiyo ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo ifikapo siku hiyo saa 6.00 usiku vituo vyote vya utangazaji vitazima mitambo yake, ambapo utakuwa mwisho wa matumizi ya mfumo wa analojia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaama jana Waziri wa Mawsiliano,Sayansi na Teknolojia Bw.Makame Mbawara, alisema kuanza hapo mfumo pekee utakaokuwa unatumika ni wa digitali.

Alisema mfumo wa digitali una umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi na utasaidia kuongeza uwekezaji kupitia simu za mikononi.

"Ili kuhakikisha tunaendana na mabadiliko ya kidunia katika masuala ya mawasiliano na teknolojia ya utangazaji, inalazimika kuanza kutekeleza mabadiliko hayo," alisema.

Aliongeza mfumo wa digitali una umuhimu mkubwa katika mawasiliano kwa sababu utaongeza ubora wa matangazo yanayorushwa na televisheni, kuwepo kwa masafa marefu pamoja na kuongeza chaneli mpya za televisheni.

"Teknolojia ya digitali ni mbadala wa teknolojia ya analojia ambayo ina manufaa makubwa hasa katika masuala ya utangazaji na kuunganisha huduma za simu," alisema.

Alitoa mwito kwa Watanzania kuanza kujiandaa na mabadiliko hayo hasa kwa kuanza kutumia ving'amuzi vitakavyowawezesha kupokea matangazo au kuanza kutumia televisheni za digitali ambazo zinapokea matangazo moja kwa moja .


No comments:

Post a Comment