24 February 2012

Polisi wanne washikiliwa Songea kwa mauaji

Kassian Nyandindi na Joseph Mwambije, Songea
SIKU moja baada ya mji wa Songea, mkoani Ruvuma, kukumbwa na vurugu kubwa zilizosababisha watu wawili kuuawa kwa kupigwa risasi, Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia askari wake wanne wa Kikosi cha Kuzuia Ujambazi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

Vurugu hizo zilitokana na maandamano ya wananchi na waendesha pikipiki za abiria maarufu kama 'yeboyebo', waliokuwa wakipinga mfululizo wa mauaji ya kikatili mjini hapa.

Maandamano hayo yalianzia katika eneo la Mjimwema hadi katikati ya mji ambapo dhamira ya waandamanaji ni kwenda katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kufikisha kilio chao kwa madai kuwa, Jeshi la Polisi mjini hapa limeshindwa kudhibiti mauaji hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Michael Kamuhanda, alisema askari waliohusika na mauaji hayo wanaendelea kuhojiwa ili kubaini uhalali wa kufyatua risasi za moto ambazo zimesababisha mauaji hayo.

“Mbali ya kuwahoji, Mkuu wa Mkoa Bw. Said Mwambungu ameunda tume ya watu nane ili kujua chanzo cha mauaji yaliyosababishwa na askari hawa.


“Jeshi la Polisi Makao Makuu, nalo litaunda tume ambayo itakuja kuchunguza tukio hili, uhalibifu uliojitokeza kutokana na vurugu hizi ni mkubwa, magari manne yaliharibiwa kwa mawe, ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa ilivunjwa mlango, madirisha na bendera za chama katika eneo la Lizaboni na Bombambili, zilichomwa moto,” alisema Kamanda Kamuhanda.

Aliongeza kuwa, uharibifu mwingine uliotokea ni nyumba ya Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Songea kupigwa mawe na kusababisha vioo vya madirisha kuvunjika.

Aliyataja maeneo yaliyoathiriwa zaidi na vurugu hizo kuwa ni Mjini Kati, Lizaboni, Bombambili, Msamala na Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa.

“Vurugu zilikuwa kubwa, zilikusanya makundi ya watu kutoka Ruhuwiko, Lizaboni, Bombambili, Msamala na Mjimwema hivyo polisi walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji ambao walikuwa wanaandama bila utaratibu.

“Ukweli ni kwamba haya maandamano hayakuwa na kibali maalumu na haijulikani yalitokea wapi, kama yangekuwa na utaratibu tungeweza kuyadhibiti bila kutumia nguvu,” alisema.

Alisema kutokana na vurugu hizo, watu 54 jana wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Songea Mjini kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo, kufanya fujo na kuharibu mali.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani hapa, imelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kuwatawanya waandamanaji na kupinda mauaji ya raia wasio na hatia yanayojitokeza mara kwa mara mjini Songea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa umoja huo mkoani hapa, Bi. Mwajuma Rashid, alisema nguvu kubwa ambayo imetumiwa na jeshi hilo, imesababisha mauaji ya watu katika maandamano hayo.

Alisema mauaji hayo ambapo yamefanywa na polisi, hayapaswi kuungwa mkono badala yake Serikali ilipaswa kusikiliza kilio cha wananchi mapema na kukifanyia kazi ili kuepuka madhara.

“Tunalitaka Jeshi la Polisi kuacha kupiga mabomu ya machozi na risasi bila utaratibu hasa katika makazi ya watu, hali hii imekuwa ikisababisha watoto wadoho wasio na hatia kuathirika vibaya.

“Mauaji ya kiatili katika mji huu, yameanza miezi minne iliyopita lakini jitihada za kupambana na wahalifu wanaohusika na vitendo hivi zilionekana kusuasua na kusababisha wananchi kujawa na jazba.

Aliongeza kuwa, umefika wakati viongozi wa Serikali, wawajibike ipasavyo katika jamii wanayoitumikia hasa wanapoletewa malalamiko na wananchi kuhusu mambo yanayowakabili katika maeneo yao kwa kuyafanyia kazi haraka bila kuchelewa.

Bi. Rashid aliwasihi vijana kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali wanapotaka kufanya maandamano ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea baadaye.

“Na wasihi sana wakazi wa mji wa Songea, tulieni katika kipindi mhiki kigumu na tushirikiane kutuliza ghasia hizi,” alisema.

Alisema umoja huo unatoa pole kwa watu wote walioguswa na mauaji hayo na kuwaomba viongozi wa mji, wahakikishe amani na utulivu unakuwepo kama ilivyokuwa awali.

Katika hatua nyingine, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepokea kwa masikitiko na kulaani mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi mjini Songea.

Chama hicho kimetoa pole kwa familia za marehemu, majeruhi, walioharibiwa mali zao na wote walioathirika kwa namna au nyingine na vurugu hizo.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Bw. John Mnyika, imesema chama hicho kinaamini mauaji hayo ni mwendelezo wa mauaji yanaendelea kufanywa na vyombo vya dola kwa nyakati tofauti nchini.

Kutokana na kukithiri kwa mauji yanayofanywa na vyombo vya dola, CHADEMA kinataka kauli kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara ya 33 ni mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

Alisema matukio ya mauaji hayo katika mikoa ya Mbeya, Mara, Arusha na mikoa mingine nchini, yameelezwa kwa kina na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Bw. Freeman Mbowe wakati wa mkutano wa nne wa Bunge mwaka 2011.

“CHADEMA kinapenda umma ufahamu kuwa, mauaji haya na mengine yanayotokea sehemu mbalimbali nchini kupitia vyombo vya dola ni ukiukwaji wa ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua uhai ni haki ya msingi wa raia wote,” alisema.

Aliongeza kuwa, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake hivyo katika mazingira ya kawaida hakuna mtu mwenye ruhusa ya kuondoa uhai wa mtu.

Alisema chama hicho kinaitaka Serikali kutoa taarifa ya ukweli kuhusu athari zilizotokana na vurugu hizo. Pia wanaitaka Serikali kueleza hatua iliyofikiwa katika uchunguzi wa vifo vyote ambavyo vimesababishwa na vyombo vya dola katika mazingira tatanishi na kuchunguza mauji yaliyofanywa na polisi mjini Songea.

“Wakati hatua za uchunguzi zikiendelea, tunataka viongozi wote wa Serikali waliohusika kusimamia kazi za vyombo vya dola zilizohusisha mauaji ya raia, wawajibike na Maofisa wa Polisi na vyombo vingine vya dola waliosababisha mauaji, wasimamishwe kazi wakati uchunguzi ukiendelea,” alisema Bw. Mnyika.



No comments:

Post a Comment