Na Salim Nyomolelo
WALIMU wapya waliopangiwa kuanza kazi katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam walalamikia uongozi wa manispaa kwa kushidwa kuwalipa fedha za kujikimu, kwa muda wa siku saba na badala yake wamelipwa siku tatu, uamuzi ambao wanadai ni kinyume na taratibu.
Wakizungumza na gazeti hili Dar es Salaam juzi, walimu hao walisema wanashangazwa na utaratibu wa manispaa hiyo kutoa fedha pungufu, wakati wenzao waliopangiwa maeneo mengine walilipwa fedha zao za kijikimu kwa siku saba.
Akizungumza na gazeti hili kwa niaba ya wenzike kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini, mmoja wa walimu hao, alidai hadi sasa wamelipwa fedha za siku mitatu badala ya saba, huku fedha zilizobaki hawaabiwi lini zitalipwa.
Alisema hali hiyo inawafanya wao kushindwa kupanga nyumba za kuishi na kununua mahitaji muhimu, jambo ambalo linawapa wakati mgumu kuripoti maeneo yao ya kazi.
"Walimu wenzetu waliopangiwa nje ya Temeke, tayari walimeshalipwa fedha na wanapanga utaratibu wa kuanza maisha mapya katika vituo vyao vya kazi, lakini sisi tunaambiwa tuchukue fedha nusu bila ya kuambiwa ni lini tutapewa zilizobaki", alilalamika mwalimu huyo.
Kwa upande wake msemaji wa manispaa hiyo, Bi.Joyce Msumba, alipoulizwa kuhusu malalamiko ya walimu hao, alisema fedha za kujikimu zinatolewa kwa siku saba, ambapo kwa walimu wenye shahada wanalipwa sh.65,000 kwa siku na wale wenye stashahada wanalipwa sh.45,000.
Bi.Msumba alisema ni kweli fedha zinazotolewa ni za siku mitatu na zilizobaki watalipwa karibuni. Aliwataka walimu hao kuwa na subira kwa sababu taratibu za kuwalipa zinafanyika.
No comments:
Post a Comment