Na Mwandishi Wetu, Mkoani
IDARA ya Mahakama na Jeshi la Polisi kisiwani Pemba limetakiwa kuyachukulia hatua makosa yanayofikishwa katika sehemu hizo ili kuwapa moyo wananchi kupitia dhana ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mwakilishi wa Jimbo la Mkoani, Bw. Abdalla Mohammed Ali katika eneo la Jondeni jimboni humo wakati wa uzinduzi wa Polisi Jamii Shehia ya Jondeni Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema, kutokuchukuliwa hatua zinazofaa dhidi ya wahalifu wanapofikishwa katika vituo vya polisi na mahakamani hali hiyo huwa inawakatisha wananchi tamaa hivyo kushindwa kushiriki ipasavyo katika shughuli za ulinzi.
Mwakilishi huyo aliwasihi wanakamati wa polisi jamii nchini kuzingatia sheria na taratibu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuepusha uvunjaji wa haki za binadamu.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Kamishina Msaidizi, Bw. Hassan Nassir Ali aliwahimiza wazazi wa Jondeni kusimamia vyema suala la maadili ikiwemo ulinzi ili kuweka mazingira yao katika hali ya usalama.
Kamanda Nassir ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alikabidhi vitambulisho kwa Wanapolisi jamii 54 ndani ya shehiya hiyo.
No comments:
Post a Comment