JUZI wanachama 1,328 wa Chama cha Wananchi (CUF), walirejesha kadi za uanachama wa chama hicho kwa madai kuwa kinaongozwa na ufalme wa sultan.
Wananchama waliorejesha kadi zao ni wa Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Matukio ya wanachama wa chama hicho kurejesha kadi za uanachama yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara tangu chama hicho kiingie kwenye mtafaruku, uliosababisha Mbunge wa Jimbo la Wawi, Bw. Hamad Rashid Mohamed, kufukuzwa uanachama.
Moja ya sababu za kufukuzwa kwa Bw. Hamad Rashid, ni kumpinga wazi wazi Katibu Mkuu wa CUf, Bw. Seif Sharif Hamad, akidai ameshindwa kuimarisha chama hicho, hivyo kukifanya kipoteze umaarufu.
Pamoja na yote haya yanayojitokeza ya kukimbiwa wanachama, viongozi wa CUF wameendelea kushirikilia msimamo wao kuwa chama hicho bado ni imara kama si ngangari.
Sisi hatuwezi kuwalazimisha waamini hivyo, lakini wenye macho tunaona kuwa CUF tuliyoifahamu miaka ya nyuma, si hii ambayo Bw. Julius Mtatiro anaitetea kwa nguvu zote.
Mgogoro ndani ya chama hicho umezidi kukidhoofisha chama hicho na si dalili nzuri kwa uhai wake. Viongozi wa chama hicho wanaweza kujidanganya kuwa wanaohama chama hicho ni mamluki, lakini sisi ambao tupo kwenye vyombo vya habari tunatambua kuwa kama juhudi hazitachukuliwa kunusuru hali hiyo, jahazi litazidi kuzama.
Matokeo ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Uzini ni moja ya dalili mbaya ya kukataliwa kwa chama hicho. Nguvu za CUF Zanzibar, kila mmoja anazifahamu. Ingawa chama hicho kina nguvu zaidi Pemba, lakini hata Unguja kilikuwa na nguvu.
Lakini kitendo cha mgombea wa chama hicho kuzidiwa kura na mgombea wa CHADEMA, ni ishara mbaya. Kuna watu wanaweza kudai kuwa CUF haina nguvu upande wa Unguja, hilo tunaweza kukiri kwamba mbele ya CCM haifui dafu, lakini kwa CHADEMA ilikuwa iking'ara zaidi.
Kwa msingi huo viongozi wa CUF wajitazame upya na si kuendelea kusisitiza kuwa chama hicho ni imara, wakati kikizidi kuporomoka.
Dhamira ya tahariri hii ni nzuri, lakini wenye mtazamo hasi watakuwa na mawazo tofauti. Kkweli ni kwamba CUF ijitazame upya kwani dalili zilizopo mbele yake zinatishia mustakabali wake.
No comments:
Post a Comment