16 February 2012

Walemavu wapewe fursa kutambua haki za msingi

Na Raphael Okello

JAMII ya watu wenye ulemavu nchini ni kundi kubwa miongoni mwa Watanzania milioni 40 ambao wamesahaulika katika sekta mbalimbali.

Ulemavu hautokani na mapenzi ya mtu fulani bali ni jambo ambalo humpata mtu bila kutegemea. Upo ulemavu wa kurithi kutoka kwa wazazi, kuugua au kupata ajali.

Wapo baadhi ya watu ambao wamepata ulemavu katika umri mkubwa wakiwa na majukumu ya kuhudumia familia. Zipo aina nyingi za ulemavu kama wa macho, ngozi, viungo au kusikia.

Katiba tuliyonayo inasema wazi kuwa ni wajibu wa Serikali kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu na wazee kwa maana kwamba huduma kwao ni wajibu na siyo msaada.

Hali imekuwa tofauti kabisa, kwani mara nyingi walemavu huwa wanapata huduma toka Mashirika ya dini na vyama vyao vya hiari vya kutetea haki zao, huku serikali ikionekana kuyaachia mashirika hayo ya dini jukumu hili muhimu.

Kwa kuwa tafsiri halisi ya mlemavu imepindishwa, basi hata sera, mikakati na hata utekelezaji wake navyo vimekuwa hivyo hivyo, jambo ambalo si haki na hatuwasaidii watu wenye ulemavu japo kwenye katiba yetu inatamkwa hivyo.

Imani potofu zinasababisha baadhi ya wanajamii wenzetu, kudhani kwamba ulemavu wa mtu unaweza kumtajirisha mwingine, kwa kumkata kiungo au kumchuna ngozi na kuipeleka kwa waganga wa kienyeji.

Kwa kuwa, hakuna dawa ya utajiri itokanayo na kiungo cha binadamu na hivyo mwenye ulemavu hawezi kutumiwa kama nyenzo ya kuleta utajiri bali yeye mwenyewe anaweza kujiletea utajiri akiwezeshwa.

Huu ni muda muafaka wa kuachana na dhana potofu kwamba ulemavu ni ugonjwa; hii inatokana na serikali  kuratibu huduma za walemavu kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Kwa nini masuala yamepelekwa Wizara ya Afya, hii ni sawa na kuchukulia kuwa Walemavu ni watu wagonjwa wanaohitaji matibabu.

Utaratibu wa huduma za walemavu kabla ya kupelekwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, walihudumiwa na Wizara ya Kazi, Vijana na Michezo.

Bw. Benson Nyasebwa ni mwezeshaji wa elimu ya uraia mkoani Mara ambaye anasema, jamii kubwa ya watu wenye ulemavu, hawajapewa kipaumbele cha elimu kutokana na jamii kubwa isiyokuwa na ulemavu, kutotambua hazi zao na kujenga shule maalumu kwa ajili ya kundi hilo.

Anasema, mlemavu anayo haki ya kumwezesha kuishi kwa kupata mahitaji yote muhimu kijamii, kiuchumi na kisiasa. Haki nyingine ni kulindwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa na kila mtu.

Anasema, walemavu wengi nchini hawatambui haki zao hivyo ni vigumu kudai haki hizo. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 20 na 21 ya mwaka 1977, inasisitiza wajibu wa Serikali kutekeleza haki hizo,

Kutokana na aina ya ulemavu alionao, ana haki ya kuajiriwa serikalini na sekta binafsi lakini kwa Tanzania, ajira kwa walemavu ni tatizo kubwa kutokana na dhana iliyojengeka kuwa, hawawezi kufanya kazi wakati wapo walemavu wenye ujuzi katika fani mbalimbali.

Anasema,  walemavu wana haki ya kushiriki uchaguzi kwa kupiga kura au kuchaguliwa kama atagombea nafasi yoyote ya uongozi kama urais, ubunge na udiwani.

Kutokana na jamii kubwa kutotambua haki zao, walemavu wamekata tamaa ya kugombea uongozi na kutoshiriki kikamilifu katika chaguzi mbalimbali hata kuhudhuria mikutano na kampeni ambayo haizungumzii ukombozi wa kundi hilo.

Anafafanua kuwa, haki zingine ambazo mlemavu anapaswa kuzipata ni usawa mbele ya sheria, kusikilizwa, haki ya kuishi, kuabudu, uhuru wa mtu binafsi, kusafiri na kutodhulumiwa mali zake.

Bw. Nyasebwa anasema, asilimia kubwa ya walemavu nchini wanakabiliwa na changamoto nyingi pamoja na kunyimwa haki zao katika kipindi cha uchaguzi.

“Watu wenye ulemavu wa kusikia hawapewe haki ya kusikiliza sera za wagombea kwa kuwekewa wataalamu wa lugha ya alama hata katika vyombo vya habari ili inapofika siku ya kupiga kura, waweze kuchagua kiongozi bora bila kujali anatoka chama gani cha siasa,” anasema.


Mkurugenzi wa Shirika la  Victoria Disability Centre, Musoma, Bw. Dannis Maina, anasema, walemavu wengi nchini, hawawezi kufikiwa na kutimiziwa mahitaji yao kutokana na ukosefu wa fedha.

Anasema,  shirika hilo, limepewa dhamana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuelimisha walemavu mkoani Mara ili waweze kutambua haki zao wakati wa uchaguzi ili kuchagua viongozi bora au kuchaguliwa katika nafasi za uongozi.

Bw. Maina anasema licha ya shirika hilo kuhudumia watu wenye ulemavu wa kusikia katika Wilaya zote za Mkoa huo, bado kuna walemavu wengi ambao hawajafikiwa kutokana na upungufu wa wataalamu wa lugha ya alama na maandishi ya nukta.

“Tumekuwa tukihamasisha watu wenye ulemavu waunde umoja wao katika ngazi ya kanda ili iwe rahisi kuwafikia wote kwa pamoja badala ya mtu mmoja mmoja jambo ambalo ni vigumu
kuwahudumia na kuwajengea uwezo.

“Baadhi yao wametoa maoni  kuwa, lipo tatizo la baadhi ya watu kuandika michanganuo ya kusaidia walemavu bila kuwashirikisha na baada ya kupata fedha, huzitumia kwa malengo yao binafsi,” anasema.

Bi. Nyasatu Manyama mkazi wa Kijiji cha Guta, Wilaya ya Bunda, mkoani humo ni mlemavu wa viungo ambaye anasema, elimu ya uraia bado haijawafikia walemavu wengi hasa vijijini hawafikiwi.

Anasema serikali inatakiwa kuwawezesha walemavu  ili kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Anasema, watapata nguvu na kuondokana na unyonge wa kudhani wao ni binadamu daraja la pili na kwamba maisha yao yataongozwa na kukaa mitaani kuombaomba na kudhani kuwa hawawezi chochote, kumbe ni fikra mbaya.

No comments:

Post a Comment