16 February 2012

Madiwani walalamikia uwajibikaji wa polisi

Na Allan Ntana, Sikonge

JESHI la Polisi wilayani Sikonge Mkoa wa Tabora, limetuhumiwa kwa ulegevu na kutowajibika ipasavyo, pale taarifa za matukio ya uhalifu zinaporipotiwa kituoni hapo.


Shutuma hizo zilitolewa wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni wilayani humo.

Wakichangia mada mara baada ya mwakilishi wa mkuu wa kituo kusoma taarifa ya utendaji ya jeshi hilo kwa kipindi cha robo ya mwaka kati ya Oktoba na Desemba, mwaka jana madiwani hao walionesha kukerwa na kitendo cha jeshi hilo kuwadai fedha za mafuta wananchi wanaoenda kuripoti matukio ya uhalifu.

Jeshi hilo limekuwa likitanguliza madai hayo kwa kisingizio kuwa pikipiki au gari halina mafuta ya kwenda kwenye eneo la tukio, madai ambayo hayakuwaingia akilini madiwani, ikizingatiwa kuwa polisi hao hao wanapoenda kukamata boda boda huwa wanaweka mafuta.

"Iweje washindwe kwenda kwenye matukio ya uhalifu," walihoji mmoja wa madiwani hao na kuongeza;

"Hali hii inawakera wananchi wetu, na ni dhahiri kwamba jeshi la polisi hapa Sikonge halifanyi kazi yake ipasavyo, huo si uwajibikaji hata kidogo, na hii ni tabia ya kuendekeza rushwa, mbona tukiwapelekea TAKUKURU  taarifa  zozote za uhalifu wanazifanyia kazi haraka?," alihoji mmoja wa madiwani hao.

No comments:

Post a Comment