24 February 2012

Tendwa achokoza nyuki CHADEMA

*Adaiwa kutumia madaraka vibaya, Lema amtupia kombora

Rehema Maigala na Queen Lema
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa, kuacha mara moja kukipigia debe Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki.

Msimamo wa chama hicho unatokana kauli aliyotoa Bw. Tendwa katika vyombo vya habari kuwa, wazee wa kimila jimboni humo wanaitaka CHADEMA na Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema, waombe radhi kwa kile alichodai, mbunge huyo aliwakejeli kwenye mazishi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu  Jeremiah Sumari.

Akizungumza na Majira Dar es salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Bw. John Mnyika, alimtaka Bw. Tendwa kutekeleza wajibu alionao kwa kuzingatia kiapo chake.

“Bw. Tendwa ameonesha upendeleo wa wazi dhidi ya  CCM kabla uchaguzi mdogo katika jimbo hili haujarudiwa, anafanya kampeni ili CCM ipate ushindi.

“Kimsingi Msajili wa Vyama vya Siasa hapaswi kutumia mamlaka aliyonayo vibaya, anafanya hivi kwa kuihofia CHADEMA itaibuka na ushindi wa kishindo,” alisema Bw. Mnyika.

Aliongeza kuwa Bw. Tendwa amekuwa na tabia za kuifanyia CCM kampeni za mara kwa mara katika chaguzi ndogo kwa lengo la kuvichafua vyama vingine vya siasa.

“Sisi tunaamini Msajili alikwenda Arumeru kufanya tathmini si kuisakama CHADEMA, propaganda za kisiasa ambazo ameanza kuzifanya zinalenga kuisaidia CCM, ameonesha uchokozi wa kisiasa ingawa yeye mwenyewe anaona ndio mbinu ya kutuchafua ili tusiibuke na ushindi katika uchaguzi huu.

“Lazima ajue chama chochote kinachosema ukweli na kufanya juhudi za kusaidia wananchi kitapendwa tu mbali ya kwamba CCM inadaiwa kuanza kampeni za chini chini,” alisema Bw. Mnyika.

Alisema kampeni hizo zinahusisha mpango wa Serikali kuanza kufufua miradi iliyokuwa imekwama ili kuwalubuni wananchi waweze kumchagua mgombea wao.

Hivi karibuni, Bw. Tendwa alidai kuzungumza na wazee wa kimila jimboni humo ambao walisikitishwa na kitendo cha Bw. Lema kukusanya vijana na kuwaonesha vidole viwili.

Alisema kitendo hicho si cha kibinadamu hasa kwa kuzingatia kuwa, vijana hao walikuwa na machungu ya kufariki kwa mbunge wao Bw. Sumari.

Wakati huo huo,  Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbless Lema, amemtaka Bw. Tendwa kuwa makini na kauli zake.

Alisema anapozungumza na vyombo vya habari, asiwe kama mtu aliyeonja kinywaji badala yake atimize majukumu yake.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Bw. Lema alisema Bw. Tendwa hapaswi kuingilia kazi za vyama vingine na kuacha propaganda za kisiasa ambazo tayari ameanza kuzionesha kwa kuzungumzia Jimbo la Arumeru Mashariki.

“Mimi kama mbunge nina haki ya kwenda kufanya kazi za kampeni, namshangaa Bw. Tendwa ila naamini alizungumza maneno haya akiwa ameonja kidogo...nasema tutapambana kufa na kupona ili tuweze kuchukua jimbo hili kwa kishindo,” alisema Bw. Lema.

Aliongeza kuwa, Msajili wa Vyama vya Siasa anapaswa kujua kuwa, mtu yeyote ambaye atapanda uovu nchini, atavuna uovu huo kwa kuwa unatembea hata katika familia zijazo.

Katibu wa CHADEMA Arusha Bw. Amani  Golugwa, alisema kauli anazotoa Bw. Tendwa si nzuri hivyo anapaswa kuwa makini.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Thobias Andengenye, alisema jeshi hilo limejiandaa kuimarisha amani na utulivu katika Jimbo la Arumeru Mashariki.



3 comments:

  1. WATU WAZIMA UNAWAONA WANA MVI,VIPARA ,UMRI MKUBWA LAKINI BADO WANAKUWA WANAFIKI MIMI NASHANGAA .MWACHE HUYO TENDWA ANATENDA KAZI YA BWANA WAKE ALIYEMWEKA PALE ASIJE AKATENDWA VIBAYA.

    ReplyDelete
  2. Mfa maji hashi kutapatapa, Hayo yote ni mikakati ya CCM kujisaidia ili kushinda Ubunge jimbo la Arumeru Mashariki. CHADEMA NI CHAMA CHA UKOMBOZI WA MTANZANIA KUTOKA KATIKA MAKUCHA YA WAROHO, WALAFI, UMIMI NA WAKANDAMIZAJI. ARUMERU WANALIJUA HILI!

    ReplyDelete
  3. Hata kama watasaidia ccm itafika mwisho wake maana watanzania siyo wa enzi hizo hawa viongozi wa ccm wanajiabisha sana mwisho wa ccm ni 2015,unafiki,uroho wa madaraka,ufisadi,uwongo,na kutokuwa makini katika kazi ndo zao,hakuna jipya.Hata mimi ni mwanaccm lakini nimechoshwa nao pia,mi siami chama lakini siwapi kura yangu.Mungu si mwanadamu.Mungu awabariki chadema.Sisi tunamwomba Mungu wetu Muumba wao wanatumia akili za kibinadamu na nguvu za kishetani.Chadema mwaka 2015 niwenu.Watu wamechoka sana na ccm pia uongozi usiomsaidia mtanzania,bali wao kujinufaisha.Riz kapata wapi pesa zote hizo na uliza pale bandarini katoa semtera 120 juzijuzi kwa pesa za nani kama siyo kodi za walalahoi.????

    ReplyDelete