Na Shaban Mbegu
KAMPUNI ya Prime Time Promotion, imesema aihusiki na sakata la kupotea kwa fedha za mapato ya mechi ya Klabu Bingwa Afrika ya timu za Yanga na Zamalek ya Misri.
Prime Time iliingia mkataba wa kusimamia mapato ya mechi ya hiyo iliyochezwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kutoka sare ya bao 1-1.
Katika mchezo huo jumla ya sh. milioni 286 zilipatikana na Yanga kupewa mgao wa sh. milioni 125.
fedha hizo zilizua mtafaruku ndani ya klabu hiyo, baada ya viongozi kuanza kushikana 'uchawi' kuwa kuna nyingine zilipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Prime Time, Joseph Kusaga alisema kampuni yake haiusiki na sakata hilo.
Alisema wao walimalizana na Yanga katika kila kitu na mapato yao waliwapa kamili kama mkataba ulivyokuwa ukisema.
"Katika hilo sisi hatuusiki hata kidogo kwani kila kitu tulimalizana na Yanga kama mkataba wetu unavyosema," alisema.
Kusaga alifikia hatua ya kutoa ufafanuzi baada ya kuulizwa swali juu hali hiyo huku wakiingia mkataba kama huo na Simba.
Katika hatua nyingine, Simba jana ilitangaza kuanzisha luninga ya klabu hiyo, Simba TV ambayo lengo lake kubwa litakuwa ni kuonesha shughuli za kila siku na matukio mbalimbali.
Akizungumza Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema Clouds Media Group kupitia Clouds TV, ndiyo watakaokuwa wakionesha vipindi hivyo vya Simba mara moja kwa wiki.
Alisema hiyo itakuwa kwa siku za mwanzoni, lakini lengo ni kuwa na televisheni ambayo itakuwa inaonesha habari za Simba saa 24 kila siku.
Kaburu alisema hiyo itakuwa ni hatua kubwa kwa klabu hiyo kongwe na itakuwa ya kwanza kuonesha njia kwa klabu nyingine.
No comments:
Post a Comment