24 February 2012

TASAF Iringa waendelea kuwanufaisha wananchi

Na Eliasa Ally, Iringa
ZAIDI ya sh.milioni 102 zitatumika kujenga mabwawa matatu katika vijiji vitatu vya Kata ya Nyang'oro, Tarafa ya Isimani iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa.

Imeelezwa kuwa lengo la ujenzi huo ni kuwawezesha wananchi katika vijiji husika kupata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kunywesha mifugo, umwagiliaji wa bustani na kusaidia katika ujenzi wa nyumba bora hali ambayo pia itawaondolea kero ya usumbufu wa kufuata maji umbali mrefu.

Akizungumza jana ofisini kwake na Majira Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Hifadhi ya Jamii (TASAF), Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Bw.Christopher Kajange alivitaja vijiji ambavyo vitanufaika na kuchimbiwa mabwawa katika tarafa hiyo kuwa ni Mangawe, Ikengeza na Mawindi kwa kuwa maeneo hayo kwa sasa yanakabiliwa na ukame unaochangia watu kutumia maji yaliyotumiwa na mifugo.

Bw. Kajange alisema, mabwawa hayo yatajengwa kwa mtindo wa kuyakinga maji yanayopatikana wakati wa masika na kuyakusanya kwa pamoja na kuweza kutumika katika msimu mzima wa kiangazi hali ambayo itakuwa ni msaada mkubwa kwa mifugo na shughuli mbalimbali za kibinadamu vijijini humo.

Pia alifafanua kuwa katika miradi ya ujenzi wa mabwawa hayo kila kijiji kati kitapatiwa sh.milioni 34 ambapo jumla yake zitakuwa sh.milioni 102 na kuongeza kuwa kati ya pesa hizo asilimia 93 zitatumika kwenye mradi husika, asilimia tano usimamizi na asilimia 1.5 zitapelekwa katika halmashauri ya kijiji.

Alisema, fedha hizo tayari zimewasilishwa na miradi hiyo katika ujenzi wake utaanza mara moja baada ya mafunzo kwa wasimamizi wa miradi hiyo kupatiwa mafunzo mahususi ya usimamizi.

Hata hivyo, Bw.Kajange aliongeza kuwa kabla ya ujenzi wa mabwawa hayo katika vijiji vya Mangawe, Ikengeza, Mawimbi kutatanguliwa na mafunzo ya usimamizi wa miradi hiyo ya ujenzi wa mabwawa, ambapo mafunzo hayo yatawalenga wajumbe wa kamati iliyochaguliwa na wananchi katika vijiji vyao.

Aidha, aliongeza kuwa katika ujenzi wa miradi hiyo wananchi watakaokuwa wanafanya kazi watanufaika moja kwa moja kwa kulipwa baada ya kufanya kazi ambapo ulipaji utakuwa kila siku baada ya kufanya kazi.

Bw.Kajange aliwataka wananchi katika vijiji vya Mangawe, Ikengeza na Mawimbi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kuwa miradi hiyo inajengwa kwa wakati unaotakiwa na kushirikiana katika shughuli za maendeleo kwa kuwa mabwawa hayo yatakuwa ni ukombozi mkubwa kwa jamii ya wananchi hao.

No comments:

Post a Comment