27 February 2012

TAMWA yaonya wazazi wanaokatisha watoto masomo

Na Rachel Balama
WALIMU  wa shule za msingi na sekondari nchini wameombwa kujiepusha na vishawishi  kutoka kwa wazazi wenye  malengo mabaya ya kuwakatisha watoto wa wasiendelee na masomo ili waolewe.

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaama jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzan(TAMWA) Bi. Ananilea Nkya

Alisema walimu wakishirikiana vema na wazazi, kutaepusha watoto wengi wa kike kukatisha masomo  ili kuolewa au kupata ujauzito na badala yake watoto hao watafanikiwa kusoma  na kufaulu.

Alisema baadhi ya Wamasai walioojiwa wamedai  kwamba watoto wao wa kike wakisoma wanabadilika na kukataa kuketekwa na kuolewa na  wanaume wenye umri mkubwa ambao ndio  wana uwezo  wa  kutoa   ng’ombe wengi kama mahari.

"TAMWA tunawapongeza  baadhi ya Wamasai ambao wamekuwa na ujasiri na  kuacha imani potofu ya kudhani kuwa kumsomesha mtoto wa kike ni hasara kwa wazazi wake eti ataishia kuolewa  na hivyo familia ya mume wake ndiyo itanufaika zaidi", ilieleza taarifa hiyo.

Alisema iko  mifano mingi  nchi nzima inayoonyesha  kuwa familia ziliosomesha  watoto wao  wa   kike  zimepiga hatua kubwa  kimaendeleo kutokana na jinsi watoto hao wanavyosaidia wazazi wao.

Alisema wameamua kutoa tamko hilo kwa sababu  mwaka huu  huu yameripotiwa
matukio  kumi kuhusu watoto wa Kimasai wanaokatishwa masomo ili waolewe kwa mahari ya ng’ombe.

Alisema njama nyingi zinafanyika ambazo ni pamoja  na kuwashawishi watoto wao   waandike majibu yasiyofaa kwenye mitihani ili wafeli wasiendelee na shule waolewe.

Matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni yalionyesha kuwa  baadhi ya
watoto waliofeli walikuwa wameandika au kuchora vitu  vya hovyo kwenye makaratasi ya
mitihani badala ya kujibu maswali waliyoulizwa.



No comments:

Post a Comment