27 February 2012

CUF yaelekea 'ICU' *Yakimbiwa na viongozi, Chama mbadala kusajiliwa leo

Grace Ndossa Dar na Benedict Kaguo, Tanga
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeendelea kusambaratika baada ya Bw. Said Miraji aliyekuwa Meneja wa Kampeni wa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Profesa Ibrahim Lipumba na aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Temeke mwaka 2010, Bw. Badau Limbu, kutangaza kujivua uanachama.

Wakati hayo yakiendelea jijini Dar es Salaam, mkoani Tanga hali ndani ya chama hicho si shwari baada ya aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Korogwe Vijijini kwa tiketi ya chama hicho, Bw. Bw. Mohamed Siu na wafuasi wengine 139, kutangaza kuachia ngazi.

Habari zaidi zinaeleza kuwa, viongozi na wanachama waliojiengua hadi sasa, leo wanatarajiwa kuwasilisha maombi ya kuanzishwa chama kipya kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw.  John Tendwa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangaza kujiengua Bw. Miraji alisema; “Leo katika maisha yangu naandika historia nyingine kwa kujivua uanachama wa CUF, awali niliandika historia kwa kuweka rehani roho yangu kwa ajili ya kutetea wanyonge katika chama nilichoamini kinasimamia haki za wananchi,” alisema.


Aliongeza kuwa, baada ya kuona chama hicho kinakufa, wao kama wanasiasa wamejipanga kusajili chama kipya na wanatarajia kuwasilisha maombi hayo leo.

“Yanayotokea CUF si kwa bahati mbaya bali yamepangwa na viongozi kwa nia ya kukidhoofisha chama hiki upande wa bara, mwelekeo wa chama hiki nilianza kuuona tangu awali ndio maana niliamua kujiweka pembeni na kufanya shughuli za ujasiliamali.

“Sikutana kuona CUF ikibomoka mbele yangu, leo hii (jana) malengo ya viongozi kubomoa chama yametimia kwa kuanza kuwafukuza watu uanachama,” alisema Bw. Miraji.

Bw. Miraji ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa CUF, aliongeza kuwa, aliwahi kumwandikia barua Mwenyekiti wa chama hicho Prof. Lipumba, miaka sita iliyopita kumtaka awashauri viongozi wa juu wabadili tabia lakini hakufanya hivyo.

Alisema Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad akiwa kama mwanzilishi wa chama hicho, ndiye anaongoza kukibomoa kwani chama kinaendeshwa bila kanuni za uendeshaji.

“Maalim Seif licha ya kuwa mwanzilishi wa chama hiki, hajui kilipo cheti cha usajili kutokana na mafanikio aliyopata katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar hivyo ameamua kuwasaliti wananchi kwa kusimamia maslahi yake bianfsi,” alisema.

Alidai viongozi waliongia katika chama hicho kwa ajili ya kukibomoa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu Bara, Bw. Julius Mtatiro, ambaye amefanikiwa kuua chama.

“Mkataba aliouingia Mtatiro wa kukibomoa chama umefanikiwa, lakini kafanikiwa kwa kuwa wenye CUF hawakuwepo, kama tungekuwepo kwenye uongozi usingekaa,” alisema Bw. Miraji.

Akizungumzia uamuzi wa chama hicho kujitoa katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Bw. Miraji alipinga sababu zilizotolewa kutosimamisha mgombea.

“Kama Arumeru Mashariki tulishika nafasi ya tatu mwaka 2010, ndiyo sababu ya kutosimamisha mgombea kwa kuhofia kupoteza pesa wakati katika kiti cha urais mwaka 2010, Prof. Lipumba naye alishika nafasi ya tatu, je, uchaguzi wa mwaka 2015 nao hatogombea urais kwa kuogopa gharama,” alihoji Bw. Miraji.

Naye, Bw. Limbu ambaye alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Temeke mwaka 2010, alisema ameamua kujiondoa katika chama hicho kwa kuwa  kimepoteza mwelekeo.

Alisema CUF imejaa ubaguzi wa Ubara na Uzanzibar ambapo uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga umedhihirisha hilo.

Huko mkoani Tanga, aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Korogwe Vijijini, Bw. Siu na wanachama wenzake 139, wamejiondoa katika chama hicho kwa madai ya kuchoshwa na kauli ya kibaguzi iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Bw. Ismail Jussa kuwa chama hicho ni kwa ajili ya Wazanzibar na waumini wa dini ya Kiisalamu peke yao.

Bw. Siu na wanachana wengine, wametangaza kujitoa ndani ya chama hicho katika Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika  Makorora wakieleza kukerwa na kauli za kuchochea udini na ukanda ndani ya chama hicho iliyotolewa na Bw. Jussa.

Alisema inasikitisha Bw. Jussa anapotangaza kuwa chama hicho kilishindwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Uzini Zanzibar kwa sababu wakazi wengi wa jimbo hilo ni wabara na wakristo.

“Kauli ya Jussa ndio imethibitisha kuwa CUF ni chama cha Wazanzibar peke yake tena Waislamu hivyo wakazi wa Bara na Wakristo hawana nafasi ndani ya chama hiki,” alisema. Bw Siu.

Alisema licha ya yeye kuwa Muislamu hawezi kukubali kauli za kibaguzi kama hizo ziendelea kushamiri ndani ya chama hicho.

Aliwataka Watanzania kutambua kuwa, CUF imepoteza dira, hivyo wasiendeleze ushabiki badala yake wapime wenyewe mwenendo wa chama na kuchukua hatua za kujiengua kwani kinachoongozwa Kisultani.

Alisema chama hicho kimekuwa kikielekeza nguvu zake visiwani Zanzibar na kutolea mfano kitendo cha mgombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Prof. Lipumba kutengewa sh. milioni 70 huku mgombea wa urais Zanzibar, akipewa sh. milioni 500 kwa ajili ya kampeni.

Kitendo hicho kinazidi kuthibitisha kuwepo ubaguzi kati ya pande mbili za muungano hivyo alimtaka Maalim Seif kujiuzulu wadhifa huo kutokana na kula kiapo cha kumtii Rais wa Zanzibar na kwamba hatatoa siri za Serikali hivyo ni wazi kuwa hataweza kuitumikia tena CUF badala yake kumtumikia Dkt. Ali Mohammed Shein.

Mmoja wa wanachama walioachia ngazi, Bw. Salim Abdala Salim, alisema amejivua uanachama kutokana na fitina zinazoendelea ndani ya chama hicho.

3 comments:

  1. Saidi Miraji si akili au mawazo yako. Itakuwa umetumwa au umerogwa

    ReplyDelete
  2. mtaishia kufukuzana hamna nia ya kuwaletea wananchi maendeleo, mmeanua kuanzisha chama kwa ajili ya ulaji tu kwani kuna vyama zaidi ya 15 mgejiunga

    ReplyDelete
  3. Politics za kijinga nchi hii. Ukikosa ulaji basi chama kibaya. haraka sana anzisheni chama chenu. wewe miraji kweli hasa ni wewe?

    ReplyDelete