16 February 2012

Sudan Kaskazini yadaiwa kuishambulia Kusini

JUBA,Sudan Kusini

WAKUU wa Jeshi la Sudan Kusini wamedai kuwa ndege za jeshi la Jamhuri ya Sudan Kaskazini zimeushambulia mji wa Jau ulioko kwenye jimbo la Unity.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Kanali Phillip Aguer, alisema mashambulizi hayo yalitokea muda wa asubuhi na mchana na wanajeshi wanne wamefariki.


Shambulizi hilo limetokea  siku chache, baada ya serikali zote mbili kutia saini mkataba wa kusitisha uhasama kati yao mjini Addis Ababa, Ethiopia.


Mji wa Jau ambao upo kwenye mpaka wa jimbo la Unity na   Kordofan Kusini, umekuwa ukigombewa  na serikali zote mbili.

Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini aliongeza kuwa wanajeshi wa serikali ya Khartoum wameongezwa kwenye mipaka yao karibu na mji huo.

Wanajeshi wa Jamhuri ya Sudan wamekuwa wakikabiliana na waasi wa kundi la SPLM-North ambao wanadai kuwa wanapata usaidizi kutoka wa serikali ya Sudan Kusini madaia ambayo hata hivyo utawala wa mjini Juba umeyakanusha  mara kadhaa.

Wadadisi wanasema ikiwa shambulizi hilo litadhibitishwa, huenda likachochea uhasama zaidi kati ya majirani hao wawili.

Ijumaa iliyopita wawakilishi wa serikali hizo walikubaliana kusitisha uhasama kati yao uliozuka baada ya mzozo kuhusu kusafirisha mafuta kutoka Sudan Kusini hadi kwenye bandari ilioko Khartoum.(AFP)

No comments:

Post a Comment