23 February 2012
Songea yachafuka
*Polisi waua waandamanaji wanaopinga mauaji ya kikatili
*Risasi za moto, mabomu yatumikia kusitisha maandamano
*Wananchi wataka JWTZ lipewe kazi ya kukomesha mauaji
*Serikali Mkoa yatoa tamko, wahalifu waanza kusakwa rasmi
Na Waandishi Wetu, Songea
SONGEA yachafuka, ndivyo unavyoweza kusema kutokana na vurugu kubwa zilizotokea jana na kusababisha watu wawili, kupoteza maisha baada ya kupigwa risasi na polisi.
Vurugu hizo zimetokana na maandamano yaliyofanywa na waendesha pikipiki za abiria 'yeboyebo', wakilalamikia kitendo cha Jeshi la Polisi mjini hapa kushindwa kudhibiti mauaji ya kikatili yaliyoanza Novemba 2011, dhidi ya watu wasio na hatia.
Kutokana na vurugu hizo, Jeshi la Polisi lililazimika kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto hali iliyosababisha mji huo kukosa utulivu, kufungwa kwa Ofisi za Serikali, masoko na maduka ya wafanyabiashara.
Kwa muda mrefu sasa, wakazi wa mji huu wamekumbwa na hofu kubwa juu ya usalama wa maisha yao kutokana na mauaji hayo ambapo hadi sasa, zaidi ya watu 10 wanadaiwa kuuawa na watu wasiojulikana.
Waandamanaji walikuwa wakiimba nyimbo za kuelezea udhaifu wa Jeshi la Polisi kwa madai ya kushindwa kazi na kuuomba uongozi wa Wilaya ukabidhi maadaraka ya ulinzi wa raia na mali zao kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ili kukomesha mauaji yaliyodumu muda mrefu.
Vurugu hizo zilianza wakati polisi wakiuondoa mwili wa mtu aliyeuawa kwa kunyongwa shingo usiku wa kuamkia jana na kunyang'anywa pikipiki aliyokuwa akiitumia kubeba abiria.
Mwili wa mtu huyo ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, ulitupwa katika Mto Mjimwema. Kutokana na hali hiyo, waandamanaji walijikusanya katika barabara inayoanzia Mjimwema hadi katikati ya mji huu.
Kifo cha mwendesha pikipiki ni mfululizo wa mauaji yanayoendelea mjini hapa ambapo Februari 20 mwaka huu, saa tatu usiku, Shekhe wa Msikiti wa Kipera, uliopo Kata ya Ruvuma, Ahmad Jamari (65), aliuawa kwa kukatwa mapanga wakati akitoka msikitini.
Kutokana na mauaji hayo, wakazi wa Kata ya Lizabon, waliandamana hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Songea, Bw. Thomas Ole Sabaya, wakilaalamikia kukithiri kwa mauaji ya wananchi wa kata hiyo yanayowafanywa na watu wasiofahamika.
Akijibu malalamiko ya wananchi hao, Bw. Sabaya alisema Serikali itaimarisha ulinzi ili kukabiliana na mauaji hayo. Februari 19 mwaka huu, mkazi wa kata hiyo Bw. Bakary Ally (20), naye aliuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.
Akizungumjza na Majira, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Dkt. Benedikt Ngaiza, amethibitisha kupokea miili ya watu wawili ambao majina yao hayajafahamika ambao walipigwa risasi na polisi pamoja na majeruhi zaidi ya 10.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Bw. Robert Banda (34), mkazi wa
Ndilima Litembo, Bw. Argerntina Mwema(40), mkazi wa Majengo, Bw. Kato Rashid (30), mkazi wa Matogoro, Bw. Issa Sandali (21), mkazi wa Mateka, Bw. Sinje Mchopa (32) na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Nyoni (53).
Wengine ni Bw. Swalehe Selemani (32), Bw. Severin Komba (45), Bi. Ester Mbali (29), mkazi wa Mshangano, Bw. Jafary Jafary (34) na Bw. Shangwe Mtaula, mkazi wa Mabatini.
Kwa upande wao, baadhi ya waandamanaji walisema kuwa, wamelazimika kuandamana ili kulishinikiza Jeshi la Polisi na uongozi wa Wilaya kukomesha mauaji hayo.
“Tulipokaribia Kituo cha Polisi mjini hapa, baadhi ya waandamanaji walianza kurusha mawe ndipo polisi walijiami kwa kupiga mabomu ya machozi na risasi za moto ili kututawanya,” walisema.
Wakati mabomu na risasi zikiendelea kupigwa, waandamanaji walipasa sauti wakilitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kushindwa kudhibiti mauaji hayo.
Tamko la serikali Mkoa wa Ruvuma
Baada ya vurugu hizo, Serikali ikoani Ruvuma, ilitoa taarifa ya kusikitishwa na tukio la kundi la vijana waendesha pikipiki za kubeba abiria kufanya maandamano katika mitaa ya Manispaa ya Songea, kusababisha vurugu na uhalibifu wa mali.
Akitoa tamko hilo, Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Said Mwambungu, alisema siku tatu zilizopita kumekuwa na tetesi za kutokea mauaji ya imani za kishirikina zinazowahusu wanawake kuondoa sehemu za mwili ili waweze kufanikiwa katika biashara zao.
Alisema kutokana na matukio hayo, Serikali ya Mkoa ulitoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo kwa kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.
Akizungumzia maandamano hayo, Bw. Mwambungu alisema, watu wawili walifariki dunia kwa kupigwa risasi wakati polisi wakitawanya waandamanaji waliokuwa wakiwarushia mawe Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
“Nawasihi wakazi wa Songea na Ruvuma, muwe watulivu katika kipindi hiki kigumu ili vyombo vya Ulinzi na Usalama viendelee kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha wote wanaojihusisha na biashara hii haramu, wanachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Alitoa mwito kwa wananchi wanaowajua watu wanaofanya uhalifu kwa njia ya uchawi na ushirikina, kutoa taarifa zao kwa viongozi wa mitaa na vyombo vya Ulinzi na Usalama mapema.
“Serikali haimini ushirikina wala uchawi, inaelewa kuhusu tiba asilia ambazo hufanywa na watu wanaopewa vibali na Serikali, wananchi wa Ruvuma kataeni ushirikina wa kiwango hiki na ramli ambazo ni chonganishi zenye lengo la kugombanisha ndugu, jamii na Taifa kwani madhara yake ni kutokea mauaji kama haya kwa watu wasio na hatia,” alisema Bw. Mwambungu.
Aliwaagiza watendaji wa mitaa, kata na tarafa kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ambalo linafanya operesheni katiika mitaa yote mjini hapa na nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wahalifu wote.
Waandishi wa habari hii ni Joseph Mwambije na Kassian Nyandindi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Poleni sana Wana Mtwara na Watanzania wote kwa misiba yote iliyowapata.
ReplyDeleteTanawasihi polisi wawe wanatumia dhana ya ULINZI SHIRIKISHI kuwabaini hao wauwaji. Wananchi wakishirikishwa kwa moyo mmoja hakuna litakaloshindikana. Bila kushirikisha jamii, hata Askari Jeshi wakipelekwa watashindwa.
Poleni Watanzania