23 February 2012

CCK: Manumba amelidhalilisha Jeshi la Polisi

*Wamtaka awajibike kwa kukanusha madai ya Dkt. Mwakyembe
Na Reuben Kagaruki

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Kijamii (CCK), Bw. Lenatus Mwabi, amesema kitendo cha Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Bw. Robert Manumba kudai kuwa ugonjwa ambao unamsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi Dkt. Harrison Mwakyembe hautokani na kulishwa sumu, kimelidhalilisha Jeshi la Polisi.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Bw. Mwabi alisema kitendo cha Bw. Manumba kukanusha madai hayo katika vyombo vya habari, kinadhihilisha kuwa utendaji kazi wake umelenga kulinda maslahi ya watu wachache badala ya Watanzania wote.

“Kimsingi DCI Manumba amelidhalilisha Jeshi la Polisi, yeye mwenyewe na watendaji wa Serikali, taarifa aliyotoa kukanusha madai ya Dkt. Mwakyembe kulishwa sumu, inaonesha yupo kwa maslahi ya watu wachache si vinginevyo,” alima Bw. Mwabi.

Alisema kutokana na hali hiyo, alimtaka Bw. Manumba awajibike kwa kutekeleza majukumu aliyonayo kisheria kwani jukumu alilonazo ni kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu ambao wanatuhumiwa kumpa sumu.

“Ukweli ni kwamba, kuna kitu kimeathiri afya ya Dkt. Mwakyembe, iweje atoke mtu nje ya maadili hadi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda amshangae, kupewa sumu zi lazima mtu anyweshwe, alichokifanya Bw. Manumba, amemdhalilisha mgongwa anayedai kulishwa sumu.

“Ni kawaida ya Jeshi la Polisi kufanyia uchunguzi malalamiko mbalimbali ya wananchi, kwa mfano, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willbroad Slaa, aliwahi kutoa taarifa ya kuwekewa vinasa sauti katika chaga za kitanda kwenye hoteli aliyofikia mjini Dodoma lakini polisi hawakufanyia kazi,” alisema.

Alisema Dkt. Mwakyembe analilalamikia Jeshi la Polisi kwa kushindwa kufanyia kazi taarifa za vitisho alivyokuwa akipata kwa kuandika barua ya siri ambayo iliishia kuchapishwa katika vyombo vya habari.

“Hii inaonesha kuwa, jeshi letu halipo kwa maslahi ya Watanzania, hivyo Bw. Manumba anapaswa kuwajibike ambapo Mkuu wa Jeshi hili IGP Mwema, apime mwenyewe.

“Bw. Manumba amewakosea Watanzania kwa kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo kwani hana mamlaka ya kuzungumzia suala zito linalohusu madai ya Dkt. Mwakyembe na kama atashindwa kuwajibika, wananchi wanaweza kuchukua hatua,” alisema.

Akizungumzia waraka unaodaiwa kusambazwa na Dkt. Mwakyembe kwa ndugu na jamaa zake wa karibu kuhusu chanzo cha ugonjwa wake, Bw. Mwabi alisema ni jambo zuri na ametumia njia sahihi.

Akizunguzia kauli zinazotolewa mara kwa mara na Waziri wa  Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta, kuwa Dkt. Mwakyembe amelishwa sumu, Bw. Mwabi, alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuwa karibu naye ili aweze kuwapata taarifa za kina badala ya kutishia kumchukulia hatua za kisheria.


Hivi karibuni, Bw. Manumba alisema kitendo cha Bw. Mwakyembe kubeza utendaji kazi wa jeshi hilo baada ya kutoa taarifa za kukanusha kuwa ugonjwa unaomsumbua hautokani na kulishwa sumu ni mawazo yake binafsi.

“Mimi siwezi kuendeleza malumbano lakini fahamu kuwa,  alichosema Dkt. Mwakyembe ni mawazo yake binafsi, hata wewe mwandishi unaweza kuzungumza chochote,” alisema Bw. Manumba.

Alisisitiza kuwa, majibu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yanaonesha kuwa, ugonjwa wa Dkt. Mwakyembe, hauhusiani na kulishwa sumu.

Akizungumzia madai ya Dkt. Mwakyembe kuwa alipeleka taarifa polisi za kutishiwa maisha yake Bw. Manumba alikiri jeshi hilo kupokea taarifa hizo na kuzifanyia kazi bila kufafanua zaidi matokeo ya uchunguzi huo.

1 comment:

  1. WABUNGE WETU MKO WAPI? HAMUONI HAYA MATUKIO YA KUFUNIKA UKWELI? (COVER UPS)BUNGE NDIO MHIMILI WA KUTETEA MASLAHI YA WATANZANIA NA KULINDA KATIBA.

    HATA AKIWA MTU MMOJA MTETEENI.

    KWENYE EPA, DOWANS, JENGO PACHA LA BOT, MIKATABA MIBOVU, HILI LA DR. MAKYEMBE, LA JAIRO.... YOTE COVER UP TUPU.

    NENDENI BUNGENI MKAIBANE MIHIMLI YA SERIKALI NA MAHAKAMA. MSITEGEMEE SISI WATANZANIA TUTASAHAU IKIWA MTANYAMAZA KIMYA.

    ReplyDelete