24 February 2012

Gumbo, Nurdin, Berko kuivaa Zamalek

Na Zahoro Mlanzi

WACHEZAJI wa Yanga Nurdin Bakari, Yaw Berko, Rashid Gumbo na Godfrey Bonny wamepona majeraha waliyokuwa yakiwakabili na sasa wapo tayari kucheza mechi ya marudiano, dhidi ya Zamalek ya Misri.

Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa Machi 4, mwaka huu jijini Cairo, Misri ambapo katika mechi ya awali iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Mbali na hao, beki Salum Telela bado anaendelea kuuguza jeraha lake alilolipata katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani alisema wachezaji hao tayari wameshaanza mazoezi mepesi, tangu mwanzoni mwa wiki pamoja na wachezaji wengine wa timu hiyo.

"Gumbo, Berko na Nurdin tayari wameanza kuimarika kutokana na kufanya mazoezi mepesi na kwa kiasi kikubwa, kama wataendelea hivyo mechi ya marudiano kama watapata nafasi ya kucheza wanaweza kufanya hivyo," alisema Sufiani.

Akimzungumzia Telela, alisema bado anasumbuliwa na kifundo cha mguu na ni mchezaji pekee, ndiye aliyebaki majeruhi lakini wengine wote wapo katika hali nzuri.

Yanga mbali na kujiandaa na mechi hiyo, pia inajiandaa na michezo ya Ligi Kuu Bara ambapo kwa hivi sasa ipo nafasi ya pili katika ligi hiyo, ikiwa na pointi 37 sawa na Simba ila zinatofautiana kwa mabao.

                                    

No comments:

Post a Comment