Na Mwandishi Maalumu, Unguja
WIZARA ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar imeeleza kuwa wakulima bado wanaendelea kuliuzia Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) zao la karafuu.
Ufafanuzi huo unatolewa zikiwa ni siku chache baada ya gazeti moja la kila siku ambalo linaandikwa kwa lugha ya Kiingereza siyo Majira, kuripoti kuwa hali ya ununuzi na uhifadhi wa zao la karafuu kisiwani Pemba hauridhishi kutokana wakulima wa zao hilo kukataa kuyauza mazao yao kwa ZSTC.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa hivi karibuni na wizara hiyo visiwani Zanzibar ilifafanua kuwa wakulima bado wanaendelea kuliuzia shirika hilo karafuu zao kama ilivyopangwa, ambapo hadi sasa jumla ya tani 588.735 zenye thamani ya sh. bilioni 8.824 zimeuzwa kwa shirika hilo kwa Wilaya ya Micheweni tu.
Aidha kwa Wilaya ya Wete jumla ya tani 1,530.536 za karafuu zenye thamani ya sh.bilioni 22.92 zimeuzwa kwa ZSTC jambo ambalo linaonesha utayari wa wakulima kuliuzia shirika hilo.
Taarifa hiyo pia ilifafanua kuwa mkulima anaruhusiwa kuhifadhi karafuu zake kwa muda apendao, iwapo karafuu hizo zitahifadhiwa katika maghala ya ZSTC na mkulima hupewa stakabadhi inayoonesha kiasi kinachohifadhiwa ambapo kwa sasa kuna idadi kubwa ya wakulima wanaotumia utaratibu huo wa kuzihifadhi na kuziuza kwa siku za usoni.
"Serikali ilichukua hatua hiyo ya uhifadhi, kwenye maghala salama ya ZSTC kwa lengo la kuziepusha karafuu kusinyaa, kupungua kwa daraja la ubora na kuziepusha kushika moto, mambo ambayo yanaweza kupelekea maafa na kumkosesha mkulima faida iwapo zitahifadhiwa nyumbani," ilifafanua taarifa hiyo.
Kuhusu madai ya bei ya karafuu taarifa hiyo ilifafanua kuwa katika bei ya soko la Dunia kilo moja inauzwa kwa dola 11 hadi 13 za Marekani.
No comments:
Post a Comment