*Polisi waanza kuwasaka Morani
*Familia yaangua kilio
Na Pamela Mollel, Arusha
JESHI la Polisi mkoani Arusha limeanzisha msako mkali wa kuwabaini vijana wa kabila la Kimasai (Morani) walioshiriki katika kumdhalilisha baba na
mwanaye, Mzee Robert Elias na Amani Robert kwa madai kuwa wamekiuka taratibu za mila na desturi katika kabila hilo.
Mafanikio hayo yanatokana na jitihada za Majira kuripoti matukio hayo mfululizo ambapo hivi karibuni Morani hao waliwadhalilisha kwa kuwapiga kwa kuwavalisha mabati shingoni, huku wakiimbiwa nyimbo za matusi kwa kuwatembeza usiku kucha bila hata kuvalia viatu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Bw.Thobias Andengenye alikiri jana ofisini kwake kuwepo kwa operesheni hiyo na tayari kuna wahalifu wawili waliohusika katika tukio hilo na watapelekwa mahakamani hivi karibuni ili sheria iweze kuchukua nafasi yake.
“Kadri tutakapokuwa tunawakamata...tutawapeleka mahakamani, ili kurekebisha hili suala la mila, tunajaribu kuwashirikisha watawala wa juu ili waweze kukaa na wadau mbalimbali nikiwa na maana ya wanasiasa, viongozi wa kimila, viongozi wa dini pamoja na makundi mengine, ili kutafuta namna nzuri ya kuendeleza hii mila," alisema Bw.Andengenye
Hatua hiyo imekuja baada ya Mzee Robert Elias na mwanaye Amani Robert kukataa kushiriki katika vikao vya kimila ambapo kundi la vijana 150 walishiriki kuwadhalilisha kwa kuhoji, kwa nini ajiondoe kwenye mila na kuamua kuokoka jambo ambalo liliwafanya vijana hao waamue kumdhalilisha.
Awali Bw.Elias alisema, kitendo alichofanyiwa na vijana hao pamoja na mwanaye Amani Robert ni sawa na unyanyasaji.
"Ni kitendo cha kinyama sana, na ni udhalilishaji mkubwa sana, hivyo ni vyema sasa Serikali ikachukua hatua badala ya kukaa kimya na kufumbia macho jambo ambalo linapelekea jamii kwa ujumla kunyanyasika," alisema
Alisema, Serikali iwasaidie kuwatenganisha Wakristo na watu wa mila kwa sababu hata katika Katiba ya nchi inaelezwa wazi kuwa kila mtu ana uhuru wa kuabudu popote.
“Mimi nimeamua kuokoka na kuwa muhumini wa Kanisa la PEFA pamoja na familia yangu, sasa wanapokuja vijana hao, na kunitaka nimkane Mungu wangu ni vigumu sana, kwa sababu Mungu alinitoa mbali na sipo tayari kushiriki suala la kimila na ninaomba wakae mbali na familia yangu na nikipata tatizo la aina yeyote wasishiriki kwa jambo lolote," alisema Bw. Elias huku akiwa anatokwa na machozi.
Aliongeza kuwa baada ya vijana hao kumkamata usiku wa Jumamosi wiki iliyopita walimtembeza usiku kucha hadi Jumapili saa 4:30 asubuhi, mara baada ya askari polisi kufika katika eneo la Burka ambapo inadaiwa kuwa vijana hao huendesha shughuli za mila.
“Wamenitukana matusi makubwa sana ya nguoni, wamenitukania baba yangu, mama yangu na hata kumtukana mtoto wangu matusi hayo hayo wakati baba ndiyo mimi, wamenitemea mate sana na kunipiga sehemu za mwili wangu huku wakiwa wametuvalisha magunia na mabati shingoni,” alisema.
Aidha baba huyo alisema kuwa amepata majeraha katika mwili wake ambapo ni sehemu ya miguu, mikono, kichwa pamoja na shingo kwa ajili ya kukatwa na bati alolokuwa amevalishwa na ndipo baada ya kuachiliwa Jumapili kwa msaada wa askari polisi alikwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru.
Kutoka na kikao kilichofanyika katika Eneo la Burka hivi karibuni, kikao hicho kiliwahusisha vijana hao pamoja na wazee wa mila ambapo walimpiga faini ya kutoa mbuzi ifikapo siku ya Jumamosi ya wiki hii.
Wananchi wa Eneo hilo la Shams walimtupia lawama Mwenyekiti wao, Bw.John Kazimoto kwa kutotoa ushirikiano juu ya suala linalomkabili Mzee Elias ambapo inadaiwa kuwa kabla ya baba huyo na mwanaye kupelekwa katika pori la Hifadhi ya Wanayamapori la Taifa (TANAPA) ili kuimbiwa nyimbo, vijana hao walimpitisha nyumbani kwa Mwenyekiti hatua iliyopelekea, Bw.Kazimoto kukaa kimya nyumbani kwake bila kutoa msaada wowote.
Hata hivyo mara baada ya Majira kumtafuta Mwenyekiti huyo ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, Bw.Kazimoto alidai kuwa wakati wa tukio hakuwepo nyumbani wala hakuwa na taarifa zozote za tukio hilo.
“Ndugu mwandishi sijaenda kumuona nyumbani kwake (Robert Elias), toka apate tatizo kama hilo, kwa sababu mara ya kwanza alipata tatizo kama hili na hakunishirikisha niseme hivi! matatizo siyo ya mtu mmoja hapa nilipo nasuluhisha ugomvi wa mke na mume, muulize vizuri kuna kitu anakuficha," alisema Bw.Kazimoto kwa hasira.
Naye Bi.Rebeca Robert alisema, kitendo alichofanyiwa mume wake na mwanaye ni dhambi hata mbele za Mungu kwa kuwa alipata maumivu makubwa hivyo anaiomba Serikali iingilie kati suala la mila kwa madai kuwa kila mtu ana uhuru wa kuabudu.
“Nilijiskia vibaya sana kwa vitendo hivyo viovu, kuvalishwa magunia na mabati shingoni huku wakiambulia kipigo kwa vijana hao ambao waliwatembeza hata bila viatu, sasa hivi mume wangu amevimba miguu kwa ajili ya kutembea juu ya mawe na miba,”alisema Bi.Robert.
No comments:
Post a Comment