23 February 2012

Ripoti ya mtoto aliyepooza yakabidhiwa

Zourha Malisa

TIMU ya madaktari iliyoundwa kufanya uchunguzi kwa mtoto, Imran Mwerangi (3), anayedaiwa kupooza baada ya kudungwa sindano ya usingizi kwa ajili ya upasuaji mdogo wa kuondoa nyama za pua, imekabidhi ripoti zake.

Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka vyanzo vya ndani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), zimeeleza kuwa ripoti hiyo imekabidhiwa juzi saa 3 asubuhi, kwa Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Melina Anjelekela.

Habari za ndani zilieleza kuwa mkurugenzi alipokea taarifa hiyo tangu juzi na kisha kuiandikia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kujua taratibu zinazoweza kufuata kwa ajili ya matibabu.

Kwa msingi huo, timu hiyo ya madaktari ilikubaliana mtoto huyo aendelea kuwa chini ya uangalizi wa hospitali mpaka wizara itakapojibu.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo ni kuwa tatizo ambalo mtoto huyo amepata ni la kudumu, hivyo atakuwa tegemezi katika maisha yake, ndiyo maana waliamua kuomba ushauri wizarani.

Mama wa mtoto huyo Bi. Amina Machulo, alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alijibu kuwa na majibu kwani ni masuala ya kitaalam zaidi, hivyo alishauri aulizwe, Dkt. Njelekela.

Juhudi za gazeti kumpata Dkt. Ngelekela ili kuzungumzia suala hilo, ziligonga mwamba baada ya kudaiwa kwamba alikuwa kwenye kikao.


No comments:

Post a Comment