Na Godwin Msalichuma, Lindi
ASASI za kiraia Wilaya ya Liwale mkoani Lindi zimetakiwa kuacha kujihusisha na masuala ya kisiasa ili kujiepusha na mwingiliano unaoweza kusababisha migogoro na migongano ya kiutendaji miongoni mwa jamii wanazozihudumia.
Mwito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Bw. Paul Chiwille katika mafunzo ya ushiriki wa asasi za kijamii kupitia mchakato wa upangaji wa bajeti inayohusu miradi ya maendeleo yaliyofanyika hivi karibuni wilayani humo.
Mafunzo hayo yaliyoshirikisha madiwani, viongozi wa asasi za kiraia watendaji wa kata na vijiji yaliandaliwa na Mtandao wa Mashirika yasiyo kuwa ya Kiserikali wilayani humo (ULIDINGO) na kufafadhiliwa na Shirika la The Foundation For Civil Society.
Bw.Chiwile alisema, lengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa asasi za kiraia ni kutoa mchango wa kimaendeleo katika sekta mbalimbali ili kuisaidia Serikali kutoa huduma katika maeneo yote ndani ya jamii kwa wakati.
“Ofisi yangu na Serikali kwa ujumla inatambua umuhimu na kuheshimu mchango mkubwa unaotolewa na asasi za kijamii, hivyo nipo tayari kuzipa ushirikiano zile zinazowajibika na kutoa mchango wa maendeleo kwa jamii,” alisema Bw. Chiwile.
Alisema, kwa kulitambua hilo viongozi wa asasi za kijamii hawapaswi kutojihusisha na shughuli za kisiasa ili kuepuka migogoro na migongano ya kiutendaji na kueleza kuwa anatarajia mafunzo hayo yaliyotolewa yatasaidia kukuza uelewa kwa viongozi na wanachama wao.
Bw.Chiwile alisema, ofisi yake itatoa ushirikano na asasi zote zitakazo kuwa tayari kufanya kazi kwa kufuata kanuni taratibu na sheria bila kuchanganya na masuala ya kisiasa kwa manufaa ya wananchi wa wilaya hiyo.
Awali Mratibu wa mradi huo, Bw. Ali Ligai alisema, mafunzo hayo yanafuatia kufanyika kwa mradi wa PETTS unaolenga ufuatiliaji wa matumizi katika rasilimali fedha za elimu ambapo uligundua kuwepo kwa mapungufu makubwa ya kutoshirikishwa kwa jamii katika uibuaji na utekaleaji wa miradi.
"Hivyo kukosekana kwa michango ya jamii katika miradi ya maendeleo," alisema.
Bw.Ligai alisema, baada ya kubaini mapungufu hayo ULIDINGO waliamua kuomba mradi mwingine wa kuwajengea uwezo wananchi katika kutoa elimu ya ushiriki wa wananchi katika upangaji mipango na bajeti.
Mratibu huyo aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo yanayoshirikisha wadau mbalimbali anategemea jamii itaweza kushiriki vyema katika uchangiaji wa miradi ya maendeleo itayoanzishwa katika kila kata wilayani humo.
No comments:
Post a Comment