27 February 2012

Dar es Salaam Quiznite’ yafana

Na Mwandishi Wetu
TUKIO la burudani la Dar es Salaam Quiznite, lililofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki lilifana kwa kiasi kikubwa ambapo burudani ya muziki na sarakasi, ziliteka washiriki waliofika katika tukio hilo.

Pamoja na burudani, tukio hilo lilihusisha mashindano ya kujibu maswali katika nyanja za muziki, michezo, elimu ya uraia na filamu ambapo washiriki waliunda makundi ya watu kumi kumi yalioingia katika mchuano.

Katika mchuano huo kundi lililojipa jina la Twiga Stars, liliibuka mshindi na kujinyakulia fedha taslimu sh. milioni 1 kutoka kwa wadhmini Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL), kupitia kinywaji chake cha Tusker Malt kama motisha ya ushiriki wao katika kujijengea ufahamu wa mambo mbalimbali duniani.

Meneja wa kinywaji cha Tusker Malt, waliodhamini tukio hilo alisema kampuni yake imefarijika na muitikio wa watu katika tukio hilo, ambalo ni jipya katika jamii ya Kitanzania.

Alisema Dar es Salaam Quiznite, imetokana na tukio la kidunia linalojulikana kama Quiznite World, linalofanyika katika nchi mbalimbali likiwa na lengo la kuwakutanisha watu wa rika mbalimbali na nyanja tofauti kwenye kubadilishana mawazo.

“Hii ilikuwa nafasi nyingine kwa wanywaji wetu kupata wigo mpana wa kuwa karibu na kinywaji cha Tusker Malt katika burudani, ambayo itawasaidia kujenga mahusiano baina yao na marafiki zao ndani ya sekta tofauti,” alisema Mchaki.

Kwa upande wake Meneja wa Quiznite World, Vincent Adour alisema anaamini uwanja huo wa majadiliano ni nafasi nzuri ya kujifunza kutoka kwa wengine, ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa kufahamiana na wakati fulani kupanua soko la biashara.

Alisema tukio hilo, sasa litakuwa linafanyika Tanzania katika kipindi cha kila robo mwaka na kwamba wanaamini litakalofuata litakuwa kubwa zaidi na kuwavutia wengi kushiriki.

"Dar es Salaam Quiznite imefungua milango kwa matukio mengine yatakayofuata, kwani tunaamini matukio yajayo yatakuwa na wigo mpana zaidi wa ushiriki," alisema Adour.


No comments:

Post a Comment