16 February 2012

Mfumo dume, elimu duni chanzo cha ukatili nchini-Utafiti

Na Jovither Kaijage, Mwanza

IMEELEZWA kuwa mfumo dume na elimu duni ya masuala ya kijamii maeneo ya vijijini hapa nchini ndizo sababu zinazochochea vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake kuendelea kushamiri ikilinganishwa na maeneo ya mijini.

Ofisa Uhamasishaji wa Shirika la Kivulini, Bi.Yusta Ntibashima aliyasema hayo jana katika Kijiji cha Mahande wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza wakati akizindua kampeni ya tunaweza kwa wakazi wa kijiji hicho.

Alisema, utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2007 katika mikoa mitatu ya Dar es Saalam, Arusha na Mbeya ulionesha kuwa maeneo ya vijiji yanaongoza kwa asilimia 56 ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto ikilinganishwa na mijini ambapo ni asilimia 41.

Alisema waathirika wakubwa wa vitendo hivyo ni wanawake kuanzia umri wa miaka 15 na pia utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 30 ya wanawake
waliofanyiwa ukatili hawakuripoti hata kuomba msaada popote kwa kuamini kuwa hiyo ni siri na kuwa ni sehemu ya maisha yao.

Kufuatia hali hiyo aliiomba Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuongeza nguvu katika suala la kuelimisha jamii hasa maeneo ya vijijini ili kuyaokoa makundi hayo na vitendo vya ukatili.

Bi.Ntibashima alisema, vitendo vya ukatili kwa wanawake vimekuwa na athari kubwa katika jamii ikiwemo kupoteza fedha na rasilimali za Taifa na hata  kusababisha vifo, ulemavu na umaskini.

Alisema, shirika hilo lilianzisha kampeni hiyo miaka mitano ya kuelimisha jamii katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara juu ya madhara ya ukatili kwa lengo la kupunguza tatizo hilo hasa vijijini.

Hata hivyo alisema, shirika hilo linaamini kuwa kama jamii ikipata elimu ya kutosha inaweza kubadilia na kukomesha vitendo hivyo ambavyo kwa kiwango kikubwa vinarudisha maendeleo nyuma kwa kupoteza nguvu kazi ya taifa.

No comments:

Post a Comment