Na Raphael Okello, Mara
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Bw.Cyprian Oyier
ametishiwa kushtakiwa mahakamani mwezi wa nne mwaka huu iwapo atashindwa kurekebisha mishahara ya walimu 422 ikiwemo kulipa malimbikizo ya madeni yanayofikia sh. milioni 25 ya walimu hao.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) wilayani Bunda, Bw.Francis Ruhumbika wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bunda na kwamba kusudio hilo limewasilishwa katika ofisi ya Mkurugenzi kwa barua yenye kumbukumbu namba, Kum.No.CWT/MR/BND.06/40 iliyotolewa Februari 13, mwaka huu.
"Pamoja na walimu hao kutorekebishiwa mishahara yao tangu mwezi Julai mwaka jana, lakini pia kuna uzembe wa kutolipwa malimbikizo ya mishahara ya walimu ambao walisharekebishiwa mishahara yao kabla ya mwaka jana," alisema Bw. Ruhumbika.
Bw.Ruhumbika alifafanua kuwa licha ya walimu hao kutolipwa kiasi hicho cha
sh.25,935,576 ambazo zilitumwa na Serikali mwezi Januari mwaka huu, walimu 14
wamefutwa madai yao huku wengine kutoonekana kwenye madai na baadhi ya vilelezo kunyofonyelewa kwenye faili.
Alimuomba Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kulipa madai yote ya walimu
yaliyohakikiwa na kwamba hawakubaliani na uhakiki wa mara ya pili.
"Tunachokisema viongozi wa CWT Wilaya ya Bunda, ni kuitisha maandamano na mgomo isiyofuata sheria kama walivyofanya madaktari tusipoona juhudi za halmashauri kurekebisha mishahara na kulipa madeni hayo yasiyohusu mishahara ndani ya mwezi mmoja kabla ya kumpeleka Mkurugenzi mahakamani," alidai.
Pia alidai licha ya changamoto zinazokaikabili sekta ya elimu, CWT wilayani humo inaomba Serikali kurudisha posho ya kufundishia kwa walimu wote nchini katika bajeti ya mwaka 2012/2013 ili kuongeza tija katika sekta ya elimu inayoonekana kudharauliwa na sekta zingine nchini.
Akijibu tuhuma hizo kwa kibali cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bw. Cyprian Oyier, Ofisa Elimu wa wilaya hiyo, Bw.Laban Bituro alisema, ofisi yake ilipokea sh. milioni 80.4, Januari mwaka huu kama malipo ya madeni ya walimu ambayo hayakuwa ya mishahara na kuwalipa walimu wote waliokuwa wakidai.
Bw.Bituro alikiri walimu 14 kutolipwa kutokana na kutowasilisha baadhi ya vilelezo vya madai hayo tatizo ambalo pia limekwamisha baadhi ya walimu kutorekebishiwa mishahara yao na kwamba hatambui madai ya walimu ya sh.milioni 25.93.
No comments:
Post a Comment