Na Michael Sarungi
HAKIKA itakuwa ni vilio vya kusaga meno kwa kizazi kijacho wakati ambapo madini, gesi, mbuga za wanyama na raslimali zote zitakapo kuwa zimekabidhiwa mikononi mwa mabepari kwa kodi za kutia aibu kwa kisingizio cha kuukomboa uchumi wetu.
Na pia, tuangalie kwa kina nini nafasi ya Mtanzania wa kesho katika Dunia ijayo bila kuwa na maliasili huku vitega uchumi vyote vikiwa tayari vikiwa mikononi mwa mabepari.
Mtanzania huyu ajaye tunatarajia ataishi vipi? Hakika huko mbele ni giza ingawa wengi wetu hatuta kuwepo lakini haya tunayo yashuhudia yakitendeka sasa hivi ni kiama kwa kizazi kijacho.
Hiki ni kiza kinene ambacho suluhu ya kukiondoa inahitaji moyo wa ujasiri na uzalendo ambao kwa kiwango kikubwa upo mikononi mwa wananachi na viongozi wao wanaobeba jukumu la kulinda maliasili.
Ukweli uliopo nchini leo ni kuwa, tumerudi katika zama za wazee akina chifu Mangungo wa Msovero na Lobengula wa Ndebele tuna kwenda bila mwelekeo huku wananchi na viongozi wetu wana lia, nani atakaye mliwaza mwenzake?
Mikataba mingi hasa ile inayo gusa raslimali za nchi yote imesainiwa na wataalamu wetu tena walioenda shule kwa namna ya kitaaluma na zaidi isiyo kuwa na pato okovu kwa uchumi na mifumo ningine iliyopo ya maisha.
Mikataba tuliyo nayo leo inatofautiana kidogo sana na ile ya akina Mangungo na wenzake ambapo, moja ya tofauti hizo ni wasomi wa leo na wazee waliongozwa na utashi.
Sababu ya pili ni kuwa, mingi ya mikataba ya sasa ni ile ya kimataifa na zilizo ridhiwa na mataifa husika yenyewe wakati wazee wetu walisaini mikataba mfu iliyo kuwa inalenga eneo husika tu na siyo nchi kama ilivyo leo.
Pia, inasainiwa wakati waafrika wengi wameenda shule na kuwa katika nafasi nzuri ya kuelewa nini kinafaa na kipi kisicho faa hii inatia mashaka juu ya uzalendo walio nao.
Wasiwasi katika mikataba hii ndiyo inayo wasababishia watu hofu na kujiuliza maswali mengi yasiyo na majibu ya kuwa nini hatima ya wajukuu zetu, je watakuwa katika hali ya gani kama kila kitu kina wanakabidhiwa wageni?
Angalia utitiri wa mikataba iliyo sainiwa nchini na mingine isiyowekwa wazi, tafiti zinaonyesha kuwa, karibia asilimia tisini ina harufu ya rushwa za kutisha.
Kuna mambo mengi ya msingi ya kuelewa juu ya haya makampuni ya kinyonyaji yanayo pora rasilimali za nchi ambapo mengi yana mkono wa moja kwa moja na wakoloni.
Ni wazi kuwa, sheria za mikataba (Laws contracts) zina sema kuwa, ni lazima pande zote zipate nafasi ya kutosha kupitia mkataba vipengele vyote kabla ya kuusaini.
Na katika mda uliotengwa, wahusika wanapata kuuangalia mkataba husika kama una maslahi ya upande wao, wakijiridhisha ndipo wataridhia kutia saini.
Mara nyingi hapa ndipo viongozi na wasomi wetu wamekuwa wakiwaacha watanzania wasiamini vile vinavyo tendwa na watendaji walio wakabidhi madaraka.
Wengi hufanya madudu na kuwaacha mamilioni ya watanzania wakibebeshwa mizigo ya madeni inayo waelemea kwani hulimbikiza mwaka hadi mwaka.
Kwa mantiki hii, mikataba mingi tuliyo nayo haiwezi kupitiwa upya kwani na masharti magumu ya kuirejea pengine kwa hisani tu ya upande wa pili.
Na kibaya zaidi kwa makampuni haya licha ya kuwa na mkono wa moja kwa moja toka mataifa ya ulaya na amerika zimesaini mikataba hii kwa zaidi ya miongo mitatu hali inayoashiria hasara kwa taifa kwa kipindi chote hicho.
Kwa ufupi ni kuwa kinacho vunwa na watanzania kutokana na mikataba mingi hii ya kipuuzi mbali na raslimali zao kuvunwa kwa wingi na kuachiwa mashimo , majanga na kudumazwa kwa uchumi ni kujidhalilisha kwa wataalamu wetu na viongozi.
Ni ukweli usio fichika kuwa, Tanzania ya leo imejaa vilio, hakuna sekta unayo weza kusema kuwa hakuna malalamiko.
Tukianza na elimu, ni uozo tu. Wanafunzi hawapatiwi mahitaji muhimu ya mabweni, hakuna walimu wa kutosha wala vitabu na maabara.
Matokeo yake ni kushuka kwa kiwango cha elimu kila kukicha, tumeshuhudia madudu kwenye matokeo ya kidato cha nne katika wiki iliyopita ambapo walifikia hatua ya kuandika nyimbo, sasa haya ni matokeo ya kukosa walimu na maadili kwa wanafunzi.
Tunatengeneza bomu ambalo likilipuka hakuna anyeweza kuuzima moto wake, vijana wanasoma katika mazingira magumu, hawawezi kuwa viongozi bora wala kujali maslahi ya nchi kama hakuna mtu anayewajali.
Njoo kwenye sekta zingine kama Nishati na Madini, hapa ni uozo unaotendeka kila kikicha, viongozi wanadiriki kuiba madini nchini na kuyaiza kwa bei ya hasara.
Kuna madini yanayozalishwa nchini pekee lakini hakuna faida kwa vijiji husika zaidi ya athari ambazo husababisha vifo kwa wananchi.
Matokeo yake wananchi wanaochimba bila vitendea kazi wanafariki na kupingiza nguvu kazi za Taifa, tutakosa watendaji wa baadaye.
Katika afya, ambayo ni muhimu kwa jamii hakuna kitu. Naipongeza serikali kwa kujenga zahanati na kusomesha madakatari, lakini je? wanapata huduma muhimu? wanafanya kazi katika mazingira ya kuridhisha?
Madaktari wana umuhimu mkubwa kama walivyo wahudumu wa ofisi. Hata hivyo, wafanyakazi wanatofautiana sana juu ya unyeti na umuhimu wa kada husika kwenye maisha ya jamii.
Achilia mbali udhaifu wa uongozi na menejimenti juu ya kushughulikia stahili na stahiki za madaktari na wafanyakazi wa sekta ya afya, kama vile: ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa na vya kisayansi; posho za kufanya kazi kwenye mazingira ya hatari; nyumba za kuishi; posho za usafiri; mazingira rafiki ya kazi ya tiba na utabibu; na mishahara inayolingana na maisha halisi, kuna tatizo sugu la siasa kutumika kuvuruga haki (za wafanyakazi, pamoja na madaktari) kwa kukwepa wajibu! Wajibu wa siasa (serikali, inayoongozwa na chama cha siasa) ni kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo ya wafanyakazi, pamoja na madaktari.
Wakati unapofika kwa wafanyakazi (pamoja na madaktari) wanapoamua kuacha kazi kwa kugoma na au kususa kufanya kazi kimbilio la wanasiasa wengi waliomo kwenye mzingo wa utawala na menejimenti ya shughuli za serikali ni kutafuta visingizio na au uchonganishi baina ya wafanyakazi na wananchi wanaohitaji huduma.
Kamwe siasa haionyeshi kushindwa hata pale wanasiasa waandamizi serikalini wanapokuwa wameshindwa kutafuta suluhisho tatizo.
Huu ni udhaifu wa serikali na sio wafanyakazi kukosa uzalendo, kwa kuwa matatizo hayo ni ya muda mrefu sasa.
Madaktari wamekuwa wazalendo muda mrefu sasa, kwanza kwa kukubali kusomea fani hiyo pia kujitoa mhanga na kutumia muda mrefu katika kujifunza na kusoma masomo hayo.
Wanatakiwa kulipwa stahiki zao ili kupunguza madudu yaliyopo.
Taaluma hii inashughulika ustawi wa afya ya binadamu, inahitaji unyeti katika kushughulikiwa na wanataaluma wenyewe na hata mazingira ya kazi.
Maliasili na Utalii na nyingine nyingi kote huko ni vituko, watu wanatafuna pesa kama hazina wenyewe hii ni dalili ya taifa lililopoteza dira na mwelekeo.
Agosti 17 mwaka 2011, Serikali kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ilitangaza bungeni kusitishwa mara kwa ukamataji na usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi.
Waziri Maige alitangaza kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi mpya wa Idara ya Wanyamapori, Obeid Mbangwa ili kupisha uchunguzi wa usafirishaji wa wanyamapori hai wenye thamani ya Sh 116 milioni Novemba 24, mwaka jana kupitia KIA.
Waziri Maige alisema bungeni kuwa, Bw. Mbangwa na maofisa wengine wawili wa wanyamapori, wamepewa likizo ya malipo hadi hapo uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili utakapokamilika.
Haijulikani ilipofikia wala mtendaji aliyechukuliwa hatua zaidi ya hizo. Tunaelekea wapi?
Hatuna majibu ya maswali yanayo tukabili kwa kuwa, yanayotolewa ni ya kupoza kutuliza maumivu na sio kuyamaliza, viongozi wameshindwa kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya wananchi na hatujui kesho hali itakuwaje.
Mfumuko wa bei umezidi kupaa, maisha ya Watanzania wengi yapo njiapanda huku baadhi yao wakilazimika kulala njaa na wengine kushindia chai kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.
Kwa mujibu wa ripoti ya bei za bidhaa iiliyotolewa na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), inaonyesha kuwa, mfumuko wa bei nchini Desemba 2011 uliongezeka hadi kufikia asilimia 19.8 ikilinganishwa na asilimia 19.2 Novemba 2011.
Kwa ujumla bei zimeongezeka hadi kufikia asilimia 121.79 Desemba 2011 kutoka asilimia 101.70 Desemba 2010.
Bei za vyakula na vinywaji baridi iliongezeka hadi kufikia asilimia 27.1 Desemba 2011 kutoka asilimia 26.1 kwa Novemba 2011.
Kwa mfano bei ya nyama jijini Dar es Salaam, ilipanda kutoka Sh 4,500 kwa kilo moja Desemba mwaka jana nakufikia kati ya Sh 5,500 na Sh 6,000 kwa sasa.
Sukari ilipanda kutoka Sh 1,800 kwa kilo Desemba mwaka jana na sasa inauzwa Sh 2,300, mchele ulipanda kutoka Sh1,550 Desemba kwa kilo hadi Sh 2,500.
Mkaa maeneo ya mijini, gunia moja lililokuwa likiuzwa Sh 20,000 sasa linauzwa kwa Sh 40,000, huku nazi moja iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh 600 sasa inauzwa kwa Sh 1,200.
Je kizazi kijacho kitatutofautishaje na akina Mangungo? Kama watu wazima wamefikia hatua ya kuuza kila kitu kilichomilikiwa na wananchi wote kama, nyumba za serikali wameuziana kwa bei ya kutupwa halafu wengi wakazigeuza kuwa baa.
Mustakabali wa wananchi umepotea, hakuna wa kumsaidia jirani yake wala hakuna dawa ya kutibu majeraha ya hali ngumu ya maisha kwa kuwa tumeshindwa kabisa kudhibiti usalama wa rasilimali zetu zinazoendelea kuchotwa usiku na mchana, tunabaki tumeduwaa.
Umeme ukipanda ni dhahiri kwamba bidhaa zote zinazozalishwa viwandani nazo zitapanda bei hasa kwa asilimia kubwa na hicho ni kilio kwa watumiaji wa kawaida.
Mazingira haya hayawezi kufuta kilio wanacholia wananchi wengi hususani wenye kipato cha chini kwa kuwa hakuna mwekezaji anayeweza kukubali kupata hasara kwa bidhaa anazozalisha, mzigo wote lazima atupiwe mtu wa chini.
Taifa limeendelea kushuhudia mwendelezo wa ajali nyingi za barabarani ambazo zimeendelea kupoteza nguvu kazi ya taifa hili.
Kuendelea kuboresha sheria za Usalama Barabarani ili zichangie katika kudhibiti shughuli za usafiri na usafirishaji,. Kutoa elimu kwa madereva ili wazingatie sheria za kanuni za kazi zao,
Umefika wakati wetu kujua kuwa wanatakiwa kuitawala nchi hii kwa misingi ya utawala bora, unao mjali mtanzania wa leo na kesho na sio kuwa makuhadi wa kampuni za magharibi.
Misingi ya utawala bora imeainishwa hata kwenye katiba yetu ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 sura ya kwanza sehemu ya 2 na 3 inayo inaeleza misingi mikuu ya malengo muhimu inayoongoza uendeshaji wa shuguli za serikali katika ngazi zote.,
Utawala bora hauishii katika chaguzi na kubadili viongozi unakwenda mbali zaidi ya hapo, huwezi kuwa na utawala bora kama hakuna nidhamu katika matumizi ya raslimali ya taifa.
Uzingatiaji uwazi na uwajibikaji kuanzia ngazi ya chini hadi taifa na hapa ndipo matatizo yanapo patikana matatizo.
Nchi yetu inakabiliwa na tatizo la uwazi mikataba mingi inayo tiwa saini na viongozi wetu huwa imejaa usiri mkubwa kana kwamba ni dhambi kwa watu wengine kujua yaliyomo na mwisho wameambulia kuumbuka.
Ni wakati mwafaka kwa watanzania kuwa na huruma na kizazi kijacho tuache ubinafsi, waasisi wa taifa hili wangekuwa na mioyo ya kilafi kama waliopo tungekuta kitu?
No comments:
Post a Comment