15 February 2012

Bima ajari kunufaisha madereva wa pikipiki

Na Makumba Mwemezi

TANZANIA ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kwa kutumia simu za kiganjani.

Teknolojia hiyo imeongeza idadi ya watumiaji kutoka 300,000 mwaka 2000 hadi kufikia laini milioni 22 mwaka jana.

Huduma iliyoboreshwa zaidi ni ya kibenki ambapo wateja wanaweza kutuma na kupokea fedha kupitia simu zao  wakati wowote.

Teknoloia hiyo imewasaidia wananchi wa vijijini ambao kwa muda mrefu hawakuwahi kupata huduma za kibenki kwa urahisi kama ilivyo sasa.

Hivi karibuni, Kampini ya Mtandao wa simu za mkononi ya Zantel imezindua maboresho katika huduma ya pesa kupitia simu za mkononi waliyokuwa wakiitoa kwa jina la Z-Pesa na sasa kuwa Ezy-Pesa.

Nilibahatika kuwa miongoni mwa waliohudhuria  uzinduzi wa mabadiliko hayo Januari 25 Mwaka huu.

Naweza kusema kwa sababu kilichozinduliwa siku hiyo, hii itabaki kuwa siku ya kukumbukwa na maelfu ya watanzania watakao nufaika na huduma mpya katika mabadiliko hayo.

Mabadiliko yaliyofanywa na Zantel yanahusu huduma iliyojulikana kama Z-Pesa; na sasa kuwa Ezy-Pesa.

Tofauti zake ni kuwa, katika Ezy–Pesa huduma zilizokuwa zikitolewa kwa mtindo wa Z- Pesa zimeboreshwa  ambapo imeongezwa huduma mpya ya malipo ya ‘bima ya ajali’ ya “Farijika”.

Bima ya ajali inatolewa kwa ushirikiano kati ya Zantel kupitia Ezy-Pesa na Shirika la Bima la Taifa (NIC) ijulikano kwa jina la “Farijika”.

Walengwa katika huduma hiyo ni  watanzania waliopo vijijini na watumiaji vyombo vya moto kama pikipiki, bajaji na baisikeli za miguu mitatu.


Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu Raisi wa kampuni hiyo, Bw. Ahmed Mokhles,ni kuwa, baada ya kujiunga mwanachama wa Farijika atatakiwa kuwa anachangia sh 150 kwa siku au 4,500 kwa mwezi, ambapo akipata ajali atapata milioni tatu kama bima ya ajali.


Bw. Mokhles anasema, pamoja na huduma hiyo, wateja wataendelea kupata huduma za kutuma na kupokea pesa, kununua muda wa maongezi, kulipia bili na huduma nyingine za kibenki kupitia simu zao.

Bw. Charles Mutalemwa, Mwenyekiti wa Bodi ya NIC anasema, zao hilo litawasaidia wakazi waliopo maeneo yasiyokuwa na miundombinu na huduma za afya.

“NIC inatoa huduma zake nchi nzima, ingawa tupo karibu mikoa yote lakini changamoto imekuwa jinsi ya kufika na kutoa huduma kwa urahisi kwa wananchi walioko vijijini, kwa ushirika huu, huduma zetu zitarahisika na tutawafikia watanzania wengi zaidi” anasema Bw. Mutalemwa.

Anasema, maeneo hayo yamekuwa yakipoteza nguvukazi kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu wanapopata ajali.

"Kupitia Farijika na Ezy-Pesa watakuwa wamepatiwa msaada mkubwa ambao utafidia gharama kubwa za matibabu yatokanayo na ajali zilizokithiri," anasema.

Ni kweli baadhi ya makundi ambayo yanatajwa kuwa miongoni mwa wanaonufaika na maboresho ya huduma za pesa kutoka Zantel, wanaamini kuwa, mpango huo utawasaidia.

Bw. Alphani Mrisho ni miongoni mwa madereva wa pikikiki jijini, anasema kuwa,  mpango huo umekuja wakati muafaka kutokana na takwimu za vyombo hivyo kuchangia kuongeza idadi ya ajali nchini.

“Ni huduma nzuri na rahisi sana kwa mwanachama kwa kuwa viwango vyake  havimuumizi  mwananchi, shilingi 150 kwa siku ni pesa ya kawaida,”. Anasema Bw.
Mrisho.

Anasema,  huduma za bima zimekuwa zikitazamwa na watanzania kama aina ya wizi au utapeli kwa kuwa, wakati mwingine mwanachama humaliza mwaka bila kupata ajali yoyote.

Anasema,  huo ni mtazamo hafifu wa kuliangalia swala la ajali kwa kuwa, wengi wamepoteza maisha kutokana na kukosa pesa za kugharamia matibabu walipopata ajali.

Maoni haya yote na mengine ambayo sikuyanukuu ni dalili kuwa wananchi wamewasikia Zantel na mpango wao wa maboresho katika huduma hiyo mpya, wasiwasi wangu ni iwapo kama wameweza au hasa wataweza kuyafikia makundi yaliyokusudiwa.

Natambua kuwa, kutoa habari za upatikanaji wa huduma hizo katika vyombo vya habari ni njia moja wapo ya kuwajulisha na kuwakaribisha washiriki, lakini jamii ya watu hawa wamezungukwa na changamoto nyingi hasa uwelewa mdogo juu ya umuhimu wa bima pamoja matumizi ya simu katika huduma hizo.

Nakubaliana na kauli ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu aliyoitoa wakati wa uzinduzi huo kuwa, matumizi ya huduma za kibenki kwa njia ya simu yanakua  nchini na yamerahisisha usafirishaji wa pesa katika maeneo ya ndani ya nchi.

Ninaamini kuwa, maboresho ya huduma hiyo na utoaji wa bima ya ajali kwa mtu mmoja mmoja kupitia farijika, utakuwa na matokeo au mwitikio chanya kutoka kwa watu wa kawaida.

Nasema hivyo kwa sababu, kwa mujibu wa taarifa kutoka Zantel, mtumiaji yeyote wa huduma hiyo atakuwa na sifa ya moja kwa moja kuwa mwanachama wa huduma ya bima ya ajali ya farijika.

Kwa sababu hii ule usumbufu ambao watu wamekuwa wakiukwepa wa kusafiri mpaka ofisi za bima na kupanga mistari kusubiri huduma utakuwa umeondolewa.

Zaidi ya urahisi huo, swala la uhuru wa mteja kuchagua, vipindi vya ulipaji wa michango yake ama kwa siku, wiki, mwezi au mwaka nalo limeongeza unafuu na utofauti wa huduma hii na pesa kupitia simu zao kwa mitambao mingine.

Naamini maboresho haya yamefanyika kwa lengo la kuwafikia kwa karibu zaidi wateja  lakini, natoa wito kuimarisha kampeni zao juu ya maboresho haya kwa kuwa, iko tabia miongoni mwetu kupokea jambo kwa shauku na kulisahau kwa muda mfupi.


Natambua watanzania tutakuwa tumewasikia, hofu yangu ni kama mtatufikia hasa sisi tulio nje ya mifumo rasmi ya huduma za bima zitolewazo ama na serikali au makampuni binafsi.

Tusiiyaache mabadiliko haya ya kheri na tija yakaishia katika vyombo vya habari,  mnatakiwa kufuatilia  na kuwashawishi ili kupata idadi ya walionifaika nayo.

Bw. Jarsh, anaeleza kuwa, zaidi ya wateja 23,000  waliokuwa wamejiunga na huduma ya Z-Pesa watahesabika kuwa wateja wa Ezy-Pesa moja kwa moja, na kuwa hadi mwishoni mwa mwaka huu wamekusudia kuwafikia zaidi ya wateja milioni moja.

Malengo haya yakitimia na Zantel ikaweza kuwafikia wateja wote basi tutakuwa na uhakika kuwa, zaidi ya watanzania milioni moja ambao mpaka sasa hawako katika mfumo rasmi wa bima watanufaika na huduma ya bima ya ajali.

Vijana wanaojishughulisha na biashara ya huduma za usafiri wa pikipiki na bajaji unaonesha kuwa, wengi wao hawana uelewa wa masuala ya bima licha ya kuwepo taarifa za huduma hizo.

Ingawa wanakubali kuwa wamekuwa wakitumia huduma ya simu, wengi wao imekuwa ni kwa ajili ya kutuma na kupokea fedha pia, kuhifadhi fedha zao badala ya kuzipeleka benki.

Pamoja na mabadiliko hayo kuwa ni sehemu ya maendeleo ya mawasiliano, ipo haja ya kuhamasishana  kuanza kuchangamkia huduma hizo.

Kwa maneno ya Naibu Waziri Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Bw.Charles Kitwanga, kupitia teknolojia, mwananchi wa Kagera atapata huduma sawa na wakati mmoja na yule wa Mtwara, na kwakuwa bima ya ajali sasa itakuwa ni uwamuzi viganjani mwa mtumiaji huduma ya Ezy-Pesa, hakuna sababu ya mtanzania kutokuwa na huduma hii.



No comments:

Post a Comment