Na Godwin Msalichuma, Lindi
MKUU wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Bw. Nurdin Babu amewataka watendaji ngazi za madiwani, wenyeviti wa serikali, kata na vijiji kusimamia vizuri suala la ardhi katika maeneo yao ili kuhakikisha akina mama wajane na wenye ulemavu wanapata haki zao.
Maagizo hayo aliyatoa wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji kutoka kata tisa za Wilaya ya Kilwa yaliyoandaliwa na Asasi ya LIWOPAK kwa ufadhili wa The foundation for Civil Society ambayo yalifanyika katika Chuo cha Maendeleo mjini humo hivi karibuni.
“Unajua migogoro mingi ya ardhi inayotokea wilayani kwetu inatokana na baadhi ya watendaji wa vijiji kutokuwa na uelewa wa sheria za ardhi...na ndiyo maana wanashindwa kufanya vikao vya kuelimisha jamii badala yake wanatumia nguvu hali inayochangia kukuza migogoro badala ya kupunguza na hivyo kufanya kuwa mikubwa,” alisema Bw. Babu.
Bw.Babu alisema, suala la migogoro ya ardhi limekuwa likisikika kila kona hapa nchini hali ambayo huwa inasababishwa na kukosekana kwa uelewa katika jamii juu ya sheria za ardhi na umiliki wake.
Mkuu huyo aliongeza kwa kuwataka madiwani, wenyeviti wa serikali na watendaji wa vijiji kusimamia vizuri suala la ardhi katika maeneo yao ili kuhakikisha akina mama wajane na wenye ulemavu hawadhulumiwi na wao kuwa wasuluhishi wa migogoro yote inayotokea katika maeneo yao.
Kwa upande wao wajumbe waliohudhuria mafunzo hayo walilishukuru shirika hilo kwa kutoa elimu hiyo na hivyo kuwapa nyenzo ya usuluhishi wa migogoro siyo ya ardhi tu bali hata mingine ya kijamii katika maeneo yao na walithibitisha kuwa wananchi wengi wa vijijini wanadhulumiwa ardhi kwa kuwa hawajuhi sheria za ardhi.
Awali Mratibu wa shirika hilo, Bw.Cosmos Bull alisema, wajumbe wengi wa mabaraza ya ardhi ambao wameteuliwa na Serikali kusimamia ardhi vijijini hawakupatiwa mafunzo ya usimamizi wa ardhi na hivyo kusababisha matatizo makubwa katika maeneo yao ambapo wameona ni bora wapatiwe mafunzo ili kuepukana na migogoro ya ardhi.
No comments:
Post a Comment