15 February 2012

Tamko la Waziri wa Elimu litekelezwe

Mhariri, Majira

NAFURAHI kupewa nafasi hii niweze kutoa dukuduku langu katika gazeti lako pendwa.
Kero yangu ni kuhusu tamko la Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi aliotoa tarehe 27.01.2012 wakati anazungumza na wakuu wa shule za msingi katika shule ya Shaban Robart kufuta masomo ya ziada.

Kwanza nampongeza sana  kwa kuliona hilo kwani hata mimi limekuwa likinikera sana hasa kitendo cha walimu kuanza asubuhi kufundisha "twisheni"  badala ya masomo ya kawaida.

Kinachonisikitisha zaidi ni kitendo cha walimu kuwachapa viboko wanafunzi pale wanapokuwa hawana shilingi 300 ya kulipia  masomo hayo.

Sambamba na hilo kila Jumatano na Jumamosi kila mwanafunzi anatakiwa kulipa sh.1200 za majaribio, bado kuna michango mingine ya kila mwezi  ambayo ni sh 300 za mengineyo mengi tu.

Mpaka hivi naandika barua limenikera sana nikiwa kama mzazi mwenye mtoto anayesoma kwenye hii shule. Lakini kwa kuwa mheshimiwa ametoa tamko kwa walimu nasubiri kuona utekelezaji kama haikuwa siasa nitaona ufuatiliaji.

Pia ninamuomba kufuatilia pale tutakapotoa taarifa za kutotekelezwa kwa agizo hilo.

Binafsi napata changamoto kubwa sana kwani watoto wangu hawataki kwenda shule bila pesa ya tution wapo tayari kwenda na pesa hiyo tu hata wao wasiwe na chochote lakini hiyo pesa ya walimu isikosekane. Tunapeleka wapi kizazi hiki?

Naomba walimu wanaohusika waelewe kwamba wazazi wengi ni maskini tunatamani kuwapa watoto wetu elimu bora lakini uwezo hatuna.

Uchumi wetu ni kama wao tu pamoja na changamoto zinazowakabili walimu wengi nawasihi wafanye bidii na kutimiza wajibu wao kwa kuwapatia elimu watoto wetu kwa mujibu wa taratibu na maadili ya kazi yao.

Ni mimi mpenda elimu
Jozema
Kigogo Dsm


No comments:

Post a Comment