16 February 2012

Ajali yasababisha maafa Kilimanjaro

Na Florah Temba, Kilimanjaro

WATU watatu wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa vibaya katika matukio mawili tofauti ya ajali za barabarani.

Miongoni mwa matukio hayo ni la gari aina ya Toyota Land Cruiser ambalo namba zake hazikufahamika, kuligonga gari lenye namba za usajili T 673 BAW Suzuki Escudo na kusababisha vifo vya watu wawili.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hizo jana, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Bw.Absalom Mwakyoma alisema, tukio la kwanza lilitokea Februari 15, mwaka huu, majira ya saa 11:30 alfajiri katika Barabara ya Moshi kwenda Arusha eneo la Maili Sita, Msasani Kata ya Kindi wilayani Moshi.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwakyoma, gari hilo la Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye hakuweza kufahamika mara moja akitokea Arusha kuelekea Moshi liligonga gari hilo la Escudo ambalo lilikuwa likiendeshwa na, Bw.Salimu Mlacha (30- 35) mkazi wa Rau.

Alisema, gari hilo lilikuwa likitokea mjini Moshi kuelekea Mirerani mkoani Arusha hali iliyosababisha gari hilo kuacha njia na kugonga mti.

Kamanda huyo alisema, baada ya gari hilo kugonga mti lilisababisha kifo cha, Bw.Peter George (28) mkazi wa Soweto mjini Moshi na mfanyakazi wa Tanzanite One Mererani aliyekuwa abiria katika gari hilo na majeraha kwa, Bw.Salimu Mlacha aliyekuwa dereva wa gari hilo ambaye alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa KCMC.

Watu wengine waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni, Bw.Emanuel Kazoka (30) mkazi wa Pasua ambaye ni fundi magari Tanzanite One Mererani pamoja na, Valeria Mushi (56) fundi ujenzi Tanzanite One mkazi wa Maili Sita ambapo wamelazwa katika Hospitali ya KCMC na hali zao zinaelezewa kuwa mbaya.

Alisema, mara baada ya ajali hiyo kutokea dereva wa Land Cruiser alikimbia na gari lake kusikojulikana na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la Land Cruiser kupita gari la mbele yake bila kuchukua tahadhari.

Hata hivyo miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya KCMC wakati juhudi za kumtafuta dereva aliyesababisha ajali hiyo zinaendelea ambapo Kamanda amemtaka dereva huyo kujitokeza ndani ya masaa 24 vinginevyo atashtakiwa kwa kosa la kutoroka.

Wakati huo huo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la, Bi.Rose Mgesa (17)mfanyakazi wa ndani katika eneo la Kiboroloni Manispaa ya Moshi amefariki dunia baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili T 910 BSR Toyota Noah PSV, lililokuwa likitokea Moshi kuelekea wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.

Kamanda Mwakyoma alisema tukio hilo lilitokea Februari 15, mwaka huu majira ya saa 12:00 asubuhi katika eneo la Meeting Point Kata ya Msaranga Manispaa ya Moshi ambapo gari hilo lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye bado hajafahamika lilimgonga binti huyo mtembea kwa miguu na kusababisha kifo chake papo hapo.

Baada ya ajali hiyo dereva alikimbia na kutelekeza gari eneo la tukio na kwamba mwili wa marehemu umehifadhia katika Hospitali ya Rufaa KCMC na chanzo cha ajali alisema kuwa ni mwendo kasi

No comments:

Post a Comment