Na Speciroza Joseph
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema sare waliyoipata Yanga ya maboa 2-2 dhidi ya Moro United, imempa matumaini ya kukaa nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa uwiano wa pointi unazidi kupungua.
Kocha huyo alisema hayo Dar es Salaam jana katika mazoezi ya kikosi hicho yaliyofanyika Uwanja wa Chamazi, kuwa matokeo hayo yamepunguza kazi kwa kuwa Yanga ni moja ya timu iliyoko juu na kupoteza kwao pointi mbili, kunaipa nafasi timu yake kuweza kukaa katika nafasi hiyo.
Azam FC kesho itacheza mechi yake ya kwanza katika mzunguko huu wa lala salama dhidi ya African Lyon kwenye uwanja huo, kama watashinda watakuwa nafasi ya tatu sawa JKT Oljoro, hivyo kupishana na Yanga kwa pointi mbili.
"Matokeo ya Yanga yana manufaa kwa Azam kwa kuwa tofauti ya pointi zinapungua, hivyo tunahitaji kushinda michezo ijayo ili kuwa katika nafasi za juu,” alisema.
Aliongeza kuwa mbali na Yanga, wanaingalia pia, JKT Oljoro ambayo imeshashinda mechi yake ya kwanza na kuvuka nafasi moja na kuwa katika nafasi ya tatu.
“Tunaangalia timu za juu na chini yetu, tunakwenda sawa, kitu kitakachotupa nafasi ni kupata ushindi katika michezo ijayo, hatutakiwi kupoteza mchezo wowote, hayo ndiyo malengo yetu katika mzunguko huu,” alisisitiza Hall.
Alisema timu nyingine iliyompa matumaini ni kupoteza kwa Mtibwa Sugar, ambao wamebaki na pointi 22 lakini kama wangeshinda wangekuwa na pointi 25, pointi ambazo timu yake ingekuwa katika kibarua kigumu kuweza kukabiliana na timu tatu za juu yake.
Azam FC ina pointi 23 iko katika nafasi ya nne, imetanguliwa na Simba na Yanga zenye pointi 28 na Oljoro yenye pointi 26, timu hiyo ipo juu ya Mtibwa yenye pointi 22 na Kagera Sugar yenye pointi 19 ikiwa katika nafasi ya sita.
No comments:
Post a Comment