23 January 2012

Wanawake waandamana kupinga kuvuliwa suruali Malawi

 BLANTYRE, Malawi

WATU takriban watu 3,000 juzi walikusanyika Blantyre nchini Malawi wakiandamana kupinga
mashambulio dhidi ya wanawake wanaovaa suruali na nguo fupi.
Baadhi ya wachuuzi wa kike wiki hii walipigwa na kuvuliwa nguo kwenye mitaa ya mji mkuu, Lilongwe na Blantyre kwa kutovaa mavazi ya asili.
Mmoja wa aliyeandaa maandamano hayo ameiambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) amewasihi wanawake kujitokeza wakiwa wamevaa suruali na fulana nyeupe kuonesha kukasirishwa kwao.
Wanawake hao walijitokeza huku wengi wao wakiwa wamevaa suruali na fulana nyeupe zilizoandikwa Peace ikimaanisha 'amani'.
Rais wa Malawi, Bw. Bingu wa Mutharika alisema kupitia redio ya taifa kuwa wanawake wana haki ya kuvaa mavazi wanayotaka.
Alikana uvumi kuwa aliamuru wanawake waache kuvaa suruali.
Mpaka mwaka 1994, wanawake kwenye nchi hiyo ya kusini mwa Afrika yenye misimamo mikali walikatazwa kuvaa suruali au sketi fupi chini ya uongozi wa kidikiteta wa Marehemu Hastings Banda.
Wanaume pia walikatazwa kufuga nywele ndefu.
Wanawake pia wamewahi kushambuliwa kwa kuvaa suruali katika nchi za Kenya, Afrika Kusini na Zimbabwe katika miaka ya hivi karibuni.
Mwandishi wa BBC aliye Blantyre, Bw. Raphael Tenthani alisema Makamu wa Rais Joyce Banda, waziri wa jinsia, wabunge kadhaa, wahadhiri wa chuo kikuu na wanaharakati ni miongoni mwa waliohudhuria maandamano ya Ijumaa.
Seodi White, mwanasheria na mwanaharakati wa haki za wanawake na aliyeandaa maandamano hayo, alisema wanawake hao hawakuvaa mavazi yasiyo ya heshima.
"Ndio Malawi ni nchi yenye msimamo mkali. Lakini tumekuwa tukivaa tunavyotaka, kwa kiwango cha heshima inayotakiwa, ambayo ni kiwango cha watu wote duniani, kwa miaka 18. Na hakuna anayeweza kusimama akasema ni kinyume na Wamalawi, " alikiambia kipindi cha Network Afrika cha BBC.

No comments:

Post a Comment