Na Kassian Nyandindi, Nionavyo.
HIVI karibuni vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti juu ya
ukatili uliofanywa na mfanyabiashara mmoja maarufu mjini Arusha, juu ya
kumnyanyasa mtoto mwenye umri wa miaka 15.
Unyanyasaji kama huu umekuwa ukipigwa vita mara kwa mara na
taasisi binafsi au za serikali ambazo zinashughulika na haki za binadamu, hivyo
kuna umuhimu mkubwa kuendelea kukemea hali hii ili jamii iweze kubadilika.
Nikirudi nyuma katika suala la udhalilishaji wa mtoto yule
ambao ulifanywa na mfanyabiashara Festo Hingi na kutokomea kusikojulikana,
inadhihirisha wazi mtu huyu? alikuwa na
nia mbaya na mtoto huyo.
Mbaya zaidi Bw. Hingi na wenzake wanadaiwa kumlawiti mtoto
huyo huku wakimfunga kamba miguuni na mikononi wakiwa wamemvua nguo na baadaye
kumpiga kwa mikanda ya suruali.
Mimi binafsi nasema huu ni unyama wa ajabu na watu wa namna
hii ni vyema wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine
wenye tabia kama hiyo.
Nasema huu ni ukatili na sasa mtoto yule wamemwachia maumivu
makali ambayo anateseka nayo wakati kiumbe hiki cha mwenyezi Mungu hakina hatia
yoyote ile.
Nampongeza Bi. Catherine Mosha ameokoa maisha ya mtoto huyo
ambapo alilazimika kumficha kwa ndugu zake ili kuepusha mpango wa kumtorosha
ambao? ulikuwa ukifanywa na watuhumiwa wa
tukio hilo kwa lengo la kufuta ushahidi mbele ya jamii na vyombo vya kisheria.
Hatua hiyo ya Bi. Mosha kufanya hivyo imefikia sasa kupata vitisho
vya aina mbalimbali kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa hivyo nashauri mama huyo
apewe nafasi ya uangalizi mzuri ili isije ikafikia mahali naye akadhurika kwa
namna moja au nyingine.
Vitisho vimekuwa vikitoka kwa ndugu wa watuhumiwa wa tukio
hilo tena kwa njia ya simu, nionavyo mimi hao wanaotoa vitisho dhidi ya mama
huyo nao wachukuliwe hatua za kisheria.
Natambua mama huyu aliamua kumsaidia mwathirika wa tukio hili
kutokana na hali mbaya aliyomkuta nayo mtoto akiwa barabarani usiku amezimia
kutokana na kipigo kilichotokana na unyama aliofanyiwa.
Nionavyo sasa ni wakati muafaka kwa mashirika yanayotetea
haki za binadamu hususani kwa watoto, hii ni fursa pekee ya kufuatilia suala
hili kwa kina na kuchukua hatua stahiki ili kukomesha vitendo hivyo.
Shirika la Action for Children(AFC) linalotetea haki za
watoto mkoani Arusha, nalipongeza kwa kutoa tamko la kulaani kitendo hiki cha
kinyama na kilichopitiliza na kuitaka jamii itambue kuwa watoto wote wana haki
sawa kwa mujibu wa sheria ya watoto ya mwaka 2009.
Sasa ni wakati muafaka kwa serikali kupitia vyombo vyake vya
sheria kufanya uchunguzi wa kutosha na wa haraka ili mtoto huyo aliyefanyiwa
unyama huu aweze kupata haki yake.
Vilevile mashirika ya kutetea haki za watoto hapa nchini tujitokeze
na kumsaidia mtoto huyu ili haki yake iweze kupatikana, na kwamba watuhumiwa
watukio hili wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa watu wengine
wenye tabia kama hiyo.
Natambua unyanyasaji kama huu ni suala ambalo limekuwa
likipigwa marufuku hata katika vitabu vyetu vya dini, hivyo mtu kama huyu
aliyefanya unyama huu kamwe hawezi kufika mbinguni badala yake amejitengenezea
shimo la dhambi.??
Kinachotakiwa sasa amrudie Mungu wake kwa kutubu makosa
aliyoyafanya ikiwemo hata mbele ya vyombo vya sheria ambavyo sasa vimekuwa
vikimtafuta kutokana na mhusika mkuu wa tukio hili kukimbia na kwenda
kusikojulikana.
Hata hivyo nasema sina shaka katika hili hata huko kukimbia
kwake iko siku atakamatwa tu mikononi mwa vyombo vya sheria ili viweze
kumchukulia hatua, na hatimaye atuambie alikuwa na lengo gani la kufikia hatua
ya kumdhalilisha na kumjeruhi mtoto huyo.
Mwandishi wa makala
haya anapatikana kwa simu namba 0712432952 au Barua pepe
nyandindi2006@yahoo.com
No comments:
Post a Comment