*Tanzania ni ya 3 duniani kwa kupokea misaada
NCHI zinazoendelea duniani, zimetakiwa kujipanga kutokana na mdororo wa uchumi ambao umeanzia nchini Ugiriki na kusambaa katika nchi za Ulaya.
Mdororo huo ulisababisha nchi za ulaya kuwa na madeni makubwa ambapo kutokana na hali hiyo, Benki ya Dunia (WB), imelazimika kutoa angalizo kwa nchi zinazoendelea ambazo zinategemea misaada kutoka mataifa makubwa duniani.
Utabiri huo umeonesha mwaka 2012, uchumi wa dunia unakua pole pole kuliko ilivyotegemewa hata kama nchi za Ulaya, zitafanikiwa kushinda mdororo huo.
Wachumi kutoka WB wamedai kuwa, uchumi utashuka kwa asilimia nne hivyo ni wazi kuwa, matarajio ya nchi maskini kupata misaada yatakuwa madogo.
Habari zilizoandikwa katika mtandao wa Financial Times, London, nchini Uingereza, Januari 18 mwaka huu, Mkuu wa Kitengo cha Uchumi kutoka WB, Bw. Andrew Burns, alikaririwa akisema nchi maskini ziombe mema pia zitegemee mabaya zaidi.
Akisisitiza umuhimu wa mpango maalumu kwa nchi maskini, Bw. Burns aliongeza kuwa, mdororo huo wa kiuchumi hautamsamehe yeyote ambapo Kukua kwa uchumi wa nchi zilizoendelea na zinazoendelea, kutashuka zaidi ukifananisha na mwaka 2008-2009.
Alisema uchumi wa dunia utayumba sana na itakuwa ngumu kukua kutokana na midororo tofauti katika vipindi tofauti.
"hii ni kwa sababu nchi tajiri duniani hazina pesa za kutosha pia zina madeni makubwa hivyo hazitakuwa na uwezo wa kusaidia nchi nyingine.
"Nchi maskini pia zina mitaji midogo zaidi, fursa mbalimbali za biashara zinazidi kupungua pamoja na misaada kutoka sekta binafsi na za umma ukifananisha na mwaka 2009," alisema Bw. Burns.
Hata hivyo, WB iligoma kubashiri matokeo ya hali hiyo na kusema kuwa, hakuna jambo linaloweza kufanyika kuzuia janga hilo.
Utabiri huo umeonesha jinsi hali ilivyo mbaya ukifananisha na juni 2011. Kwa kutegemea na kununua fedha sokoni, uchumi wa dunia unaweza kukua kwa asilimia asilimia 2.5 mwaka huu asilimia 3.1 mwaka 2013.
Inatarajiwa kuwa, uchumi wa Ulaya utashuka kwa asilimia 2.1 mwaka 2012 ambapo hali hiyo inasababishwa na matukio mbalimbali yaliyopita katika nchi zenye uchumi mkubwa.
Tukio hilo litasababisha biashara ya dunia kushuka na kuathiri uchumi wa nchi zinazoendelea hivyo mahitaji ya nchi maskini yatapungua.
"Injini ya uchumi wa dunia haswa nchi zinazoendelea inakwenda pole pole sana wakati ambao hata uchumi wa Umoja wa Ulaya uko katika hali mbaya, hali hii itaambukiza maeneo mengine," alisema Bw. Burns.
Aliongeza kuwa, kama hali itakuwa hivyo nchi zinazoendelea hazitafanikiwa kupata misaada kutoka nchi za Ulaya ambazo nyingi zitaumizwa kutokana na kuanguka kwa bei ya mafuta na mazao ya biashara.
Alisema suala la kuhamisha fedha kutoka kwa waafrika waishio Ulaya kupeleka nchi wanazotoka hususani ndugu zao, litapungua kwa asilimia tano kutokana na pato la nchi tajiri kushuka.
Benki za Afrika nazo zitakuwa katika wakati mgumu kwani benki nyingi katika nchi zinazoendelea, zina mikopo ambayo mingi inafikia mwisho wake mwaka 2012.
China ni nchi pekee kati ya nchi zenye uchumi mkubwa duniani ambayo itaweza kupambana na tatizo hilo lakini nchi zenye uchumi wa kati zitayumba sana ukifananisha na yaliyotokea mwaka 2008.
Mwaka 2008, kulitokea mdororo mkubwa kiuchumi duniani ambao chanzo chake ni mikopo mikubwa ambayo ilitolewa katika sekta ya nyumba.
Nyanja nyingine za kukuza uchumi, zikiendelea kukua pole pole na kusababisha kushuka kwa mahitaji duniani.
Kutokana na hali hiyo, Marekani ndio nchi inayongoza duniani kwa kutoa misaada mingi.
Hadi sasa, nchi hiyo imetoa zaidi ya sh. bilioni 35 (sawa dola za marekani milioni 21.787), Ujerumani inashika nafasi ya pili kwa kutoa zaidi ya sh. bilioni 19.6 (sawa na dola za Marekani milioni 12.291).
Wengine ni Ufaransa ambayo inashika nafasi ya tatu kwa kutoa zaidi ya sh. bilioni 15.8 (sawa na dola za Marekani milioni 9.884), Uingereza inashika nafasi ya tano kwa kutoa sh. bilioni 15.7 (sawa na Dola za Marekani milioni 9.849).
Japan inashika nafasi ya sita kwa kutoa zaidi ya sh. bilioni 12.2 (sawa na dola Marekani milioni 7.679).
Uchambuzi huo unaonesha mchanganuo wa nchi kwa mujibu wa mtandao wa Visual Economics, hivi karibuni.
Kwa mujibu mtandao huo, Umoja wa Ulaya ungechukua nafasi ya pili kwani imetoa misaada isiyopungua sh. trilioni 18.8 (sawa na dola za Marekani bilioni 11.774)
Katika mchanganuo huo, nchi inayoshika nafasi ya kwanza kupokea misaada mingi duniani kutoka Marekani ni Iraki.
Itakumbukwa kuwa, Marekani na washirika wake waliivamia nchi hiyo miaka tisa iliyopita na kumkamata kiongozi wake Sadam Hussein hivyo kusababisha umaskini mkubwa.
Umaskini huo ulichangiwa na uharibifu wa miundombinu pamoja na makazi ya watu. Nchi hiyo imepokea trilioni 6.825 (sawa na dola za Marekani bilioni 4.266), ikifuatiwa na Afghanistan iliyopokea trilioni 2.33 (sawa na dola za Marekani bilioni 1.45).
Afghanistani nayo ilihusishwa na migogoro ya kivita kutokana na magaidi wa Al qaeda kujificha katika nchi hiyo, hata hivyo kiongozi wa kundi hilo, Osama Bin Laden, aliuwawa chini ya utawala wa Rais wa Marekani Bw. Barak Obama mwaka 2011.
Nchi ya tatu ni Sudan ambayo imepokea bilioni 1.16 (sawa na dola za Marekani milioni 725), ikifuatiwa na Colombia iliyopokea bilioni 899 (sawa na dola za Marekani milioni 562).
Nchi ya tano ni Misri ambayo imepata bilioni 865 (sawa na dola za Marekani milioni 541) na ya sita DRC Congo iliyopokea bilioni 777 (sawa dola za Marekani milioni 486).
Inayofuata ni Pakistani ambayo imepokea dola za Marekani milioni 465, Nigeria ikishika nafasi ya nane kwa kupokea dola za Marekani milioni 414.
Ethiopia inashika nafasi ya tisa kwa kupokea dola za Marekani milioni 344 na nchi ya mwisho katika orodha ya 10 bora ni Kenya ambayo imepokea dola za marekani milioni 304.66666666
Nchi 20 zinazopokea misaada ya maendeleo duniani, inayoongoza ni Iraki ambayo imepokea dola za Marekani bilioni 9. Nchi ya pili ni Afghanistan iliyopata dola za Marekani bilioni 3.951.
Tanzania ni nchi ya tatu ambayo imepokea dola za Marekani bilioni 2. 811, nchi ya nne ni Vietnam, ambayo imepokea dola za Marekani bilioni 2.497.Ya tano ni Ethiopia iliyopokea dola za Marekani bilioni 2.422
Nchi ya sita ni Pakistan iliyopokea dola za Marekani bilioni 2.212, Sudan iliyopokea dola za Marekani bilioni 2.104, Nigeria dola za Marekani bilioni 2.042, Cameroon dola za Marekani bilioni 1.933. Nchi ya mwisho katika 10 bora ni Palestina, iliyopokea dola za Marekani bilioni 1.868.
Nyingine ni Msumbiji ikiwa ni nchi ya 11 kupokea dola za marekani bilioni 1.777, Uganda dola za Marekani bilioni 1.728, Bangladeshi dola za Marekani bilioni 1.502 na China ilipokea dola za Marekani bilioni 1.439.
India ilipokea dola za Marekani bilioni 1.298, Kenya dola za Marekani bilioni 1.275, Ghana dola za Marekani bilioni 1.151, Morocco dola za Marekani bilioni 1.090 na Misri dola za Marekani bilioni 1.083.
No comments:
Post a Comment