Na Mwandishi Maalumu, Kigoma
VIJANA wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Operesheni ya Miaka 50 ambao wamehitimu
mafunzo ya awali ya kijeshi Kambi ya JKT Bulombora wameiomba Serikali chini ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Kikwete kudumisha mafunzo yake kwa maelezo kuwa ni moja ya vyanzo vianavyochangia kuimarisha mshikamano na udugu wa kitaifa hapa nchini.
Waliyasema hayo juzi mkoani Kigoma huku wakifafanua kuwa uelekeo wao hivi sasa, baada ya kuhitimu mafunzo ya JKT katika kambi hiyo umeboreka na kustaarabika tofauti na vijana waliopo vijijini na mijini ambao hawakufanikiwa kupitia JKT na wanaendelea kujihusisha dhidi ya vitendo viovu vinavyochangia kuhatarisha amani miongoni mwa jamii.
Akisoma risala ya vijana hao miongoni mwa Askari hao, Nuru Adamu kwa niaba ya wahitimu wenzake mbele ya mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Issa Machibya, wakati wa hafla ya ufungaji mafunzo ya JKT Bulombora alisema uelekeo wao sasa umebadilika.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, uelekeo wetu hivi sasa ni tofauti kulinganisha na vijana wenzetu ambao hawajapitia JKT, hivyo tunaiomba Serikali kuhusu suala la JKT liwe la lazima kwa vijana wanaomaliza elimu ya kidato cha nne, sita na vyuo wapitie JKT," alisema.
Vijana hao waliishukuru Serikali kwa kurejesha mafunzo hayo, kwani yamewasaidia kujitambua tofauti na hapo awali yaliposimamishwa mwaka 1994 kwa sababu mbalimbali za kiuchumi na waliahidi kuyanzingatia zaidi kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Awali Mkurugenzi wa Utawala wa JKT, Luteni Kanali Eslom Lubinga, aliwakumbusha wahitimu hao na wananchi kwa ujumla kwamba, lengo la kuanzishwa JKT Julai 10 mwaka 1963 lilikuwa ni kujenga utaifa, uzalishaji mali na kuandaa Jeshi la Akiba tayari kukabiliana na maafa na adui atakayethubutu kujipenyeza na kuhatarisha amani ya nchi.
Aliongeza, JKT ni jando la kitaifa linalowaunganisha vijana wa Tanzania pamoja bila kujali tofauti zao na kuwapatia mafunzo ya awali ya kijeshi, malezi yenye utamaduni wa taifa na stadi za kazi zinazowawezesha kujitegemea na kuajiriwa katika sekta za umma.
Akifafanua zaidi, Luteni Kanali Lubinga alisema, askari wanapaswa kuheshimu sheria na kuwa tayari kuelimisha umma katika hoja za msingi na zenye utata kwa nidhamu, uadilifu na unyenyekevu.
"Askari ni mtu aliyeteuliwa miongoni mwa jamii na kupewa mafunzo maalumu kwa ajili ya kulinda na kutetea umma na tabaka tawala," alisema
Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yalijikita katika kutoa elimu ya afya, madhara ya wizi, ulevi, dawa za kulevya na Ukimwi hali iliyochangia kuleta utulivu na mbadiliko ya kitabia kwa vijana hao.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Mafunzo na Malezi JKT Bulombora, Meja Damian Sanga alisema mafunzo yalifunguliwa Julai 26 mwaka jana, ambayo yaliwashirikisha jumla ya vijana 721.
Meja Sanga aliongeza kuwa kati yao wavulana walikuwa 558, wasichana 163 na 10 miongoni mwao hawakumaliza mafunzo hayo kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro, hivyo kufanya waliohitimu kuwa 710, wavulana 549 na wasichana 161.
No comments:
Post a Comment