Na Heckton Chuwa, Kilimanjaro
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw.Leonidas Gama, ameagiza uongozi wa Wilaya ya Moshi na Hospitali ya Rufaa ya KCMC,
mkoani humo kuhakikisha kuwa wagonjwa kutoka nje ya nchi ambao huwa wanafika kupata tiba katika hospitali hiyo wanaingia nchini kwa kufuata taratibu halali.
Bw.Gama alitoa agizo hilo juzi wakati wa ziara yake hospitalini hapo, ambapo pamoja na changamoto nyingine alizokutana nazo ni ile ya ongezeko kubwa la wagonjwa kutoka nje ya nchi wengi wao wakidaiwa kuingia nchini bila kufuata taratibu hivyo kuchangia msongamano.
“Kuna taarifa kuwa, wengi wa wageni hawa hawafuati taratibu za kisheria kuingia nchini, kufuata matibabu huku wakitumia mawakala maalumu, tena wanakaa kwa kati ya wiki moja na miezi miwili huku wakiandamana na jamaa zao, hii ni mbaya kiuchumi na kiusalama pia. Hii ni hatari kwa usalama zaidi kwa maana wenye nia mbaya na nchi yetu watatumia mwanya huu kuingia mchini kutekeleza nia zao mbaya," alisema.
Bw.Gama alisema, serikali mkoani humo haitavumilia suala hilo liendelee na kwamba italivalia njuga kwa vile tayari wana majina ya mawakala hao ambao alisema ni pamoja na wamiliki wa baadhi ya nyumba za kulala wageni zilizopo maeneo mbalimbali mkoani humo.
Mkuu huyo, aliahidi kuwa uongozi wa Mkoa utatoa ushirikiano kwa hospitali hiyo kutekeleza swala hilo na majukumu mengine ambapo pia alitoa wito kwa wananchi wote wenye mapenzi mema kutoa ushirikiano kwa ofisi yake na hospitali ya KCMC katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Moshy Ntabaye, alisema uongozi wa hospitali hiyo una taarifa ya wagonjwa wanaokuja kutoka nje ya nchi na ambapo alikiri kuwa ni changamoto kwa hospitali hiyo.
“Wengi wanatoka nchi jirani na wanaongea lugha ya Kiswahili na wanajua maeneo karibu yote yanayoizunguka wilaya yetu hivyo kujitambulisha ni wa kutoka maeneo ya hapa mkoani. Tayari tumeanza kulishughuikia suala hilo kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi na idara ya uhamiaji mkoani hapa,” alisema.
Kuhusu msongamano wa wagonjwa, Dkt.Ntabaye alisema uongozi wa hospitali hiyo unatarajia kujenga wodi mpya ya kawaida itakayokuwa na vitanda 200 ili kupunguza adha hiyo.
No comments:
Post a Comment