Na Peter Mwenda, Pemba
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimekubaliana na wananchi waliotoka Kisiwa cha Pemba kuchanga sh. 100
kila wiki kwa ajili ya maendeleo ya kisiwa hicho.
Uamuzi huo umefikiwa jana baada ya kufanyika kwa mkutano wa viongozi wa ngazi zote kutoka wilaya nne za Pemba na kuamua kuanzisha mfuko maalumu ambao fedha zitakazokusanywa, zitatumika kushughulikia changamoto zinazoakabili kisiwa hicho.
Mfuko ambao utatumika kukusanya fedha hizo utafahamika kwa jina la shilingi 100 kutokana na fedha ambazo kila wananchi aliyefikia umri wa miaka 18 atachangia.
Akizungumza na viongozi hao, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alisema kuwa, umefika wakati kwa wananchi wa Pemba kuchanga fedha zao bila kushirikisha serikali kwa ajili ya maendeleo.
"CUF imefanya makubwa katika siasa hasa Pemba kutoka Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, chaguzi zote tumechukua kila kitu sasa tuangalie upande wa pili wa maendeleo, tumeingia serekalini lakini serikali haiwezi kufanya kila kitu, Kilimanjaro na Arusha wamefanya maendeleo yao wenyewe, je sisi hatuwezi?" aliuliza Maalim Seif.
Alisema kuwa, wananchi wa Kisiwa cha Pemba wanatakiwa kutambua kuwa, wamefanikiwa kwa asilimia kubwa katika kujenga siasa lakini sasa wanatakiwa kubadili mtazamo na kuangalia katika kujenga uchumi wao.
Aliwaambia viongozi hao kuwa, kwa kutumia ushawishi wa kisiasa wanaweza kutumia fursa hiyo kuhimiza maendeleo yao ili kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kutolea mfano kuwa, fedha hizo zitasaidia katika kuboresha elimu, afya, miundombinu na barabara.
"Watafiti wa masuala haya wanasema kuwa, Pemba wakiamua wanaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo maana wananchi watashiriki kikamilifu baada ya kutolewa elimu," alisema Maalim Seif.
Kuhusu mfuko huo kujenga taswira tofauti kwa wananchi alitumia nafasi hiyo kuwatoa hofu wananchi kuwa, sera ya serikali inahimiza wananchi kuchangia maendeleo yao hivyo hakuna kitu kipya katika hilo na haoni kama kutakuwa na tatizo lolote.
Alisisitiza kuwa, CUF imekuwa ikishinda katika chaguzi mbalimbali na kutoa viongozi karibu wote kutoka chama hicho hivyo kwa kutumia nafasi hiyo, wanaweza kufanikiwa na kwamba, hakuna sababu ya kushirikisha kiongozi wa serikali katika kufanikisha utaratibu huo.
Maalim Seif alisema kuwa katika kufanikisha hilo, wameamua kutoa wiki sita kwa kamati na watalaamu ambao ndiyo wanaofanikisha kuanza kwa mfuko huo kujipanga na kisha baada ya muda huo watatakiwa kutoa uamuzi wa walipofikia ili sasa kuweza kuwajilisha wananchi.
Awali Mbunge wa Jimbo la Chakechake, Mussa Haji Kombo alisema, alikaa na watalaamu mbalimbali na kubaini kuwa, kama wananachi wa Pemba watachanga sh.100 watakusanya fedha nyingi ambazo zitasaidia katika kujenga Pemba yenye maendeleo makubwa.
No comments:
Post a Comment