*CTI yatoa tamko, wanaharakati waipinga, NCCR kuandamana
Agnes Mwaijega na Rose Itono
SHIRIKISHO la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), limetoa tamko la kupinga ongezeko la bei ya umeme
ambalo limepitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA),.
Inadaiwa kuwa, ongezeko hilo litaathiri wananchi na kusababisha bidhaa zinazozalishwa nchini, kushindwa kuhimili ushindani wa soko ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CTI, Bw. Felix Mosha, alisema kiwango kilichoongezwa ni kikubwa, ukilinganisha na nchi nyingine ambazo Tanzania inashirikaiana nazo kibiashara.
Asilimia 42.2 iliyotangazwa na EWURA ni kubwa ukilinganisha na nchi za Uganda, Kenya na Rwanda, sisi tunasisitiza kiwango hiki ni cha juu, Serikali inapaswa kuangalia na kukipunguza ili mauzo ya bidhaa zetu katika masoko ya nje yasishuke,¡± alisema.
Alisema kwa hali ilivyo sasa, bidhaa za Tanzania zitauzwa bei ya juu ili kufidia gharama za uzalishaji na matokeo yake zitashindwa kununulika.
Aliongeza kuwa, Serikali ina uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme wenye gharama ndogo ambao hautaumiza Watanzania hasa wafanyabiashara.
Nchi ambazo tunashirikiana, wanazalisha umeme wa kiwango cha juu, lakini gharama zao si kubwa kama hapa kwetu, Serikali inapaswa kuangalia hali ya uchumi wa nchi na wananchi wake kama wana uwezo wa kugharamaia umeme kwa kiwango hicho kikubwa.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapaswa kupunguza matumizi na kushusha kiwango cha madeni, alisema Bw. Mosha.
Wakati CTI ikitoa tamko la kupinga nyongeza hiyo, wanaharakati wamezidi kupigilia msumari uamuzi wa EWURA kwa madai kuwa, utayumbisha watumiaji na wasiotumia nishati hiyo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Dar es Salaam jana na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bi. Mary Nsemwa, ilisema gharama za uzalishaji zitapanda na walaji maskini kwa matajiri watahitaji kufidia wazalishaji.
Alisema ongezeko la bei ya umeme litachangia ugumu wa maisha kwa Watanzania maskini na litawahusu wateja wa hali ya chini, wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi.
Swali la kujiuliza, akina nani wanaotumia umeme chini ya uniti 50 katika hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida?" alihoji Bi. Nsemwa na kuongeza kuwa ni mara chache kupata watu wanaoangukia kwenye kundi hilo lakini kupanda kwa bei ya umeme hata kwa wale ambao hawatumii umeme mwingi, kutawaathiri kwani kunapandisha gharama ya vitu vingine.
Alisema TGNP imefuatilia na kubaini wanaoumia ni watumiaji wa umeme majumbani ambao wanatumia chini ya uniti 50.
Wakati huo huo Chama cha NCCR-Mageuzi, leo kinatarajia kufanya maandamano kwenda Ofisi za Tume ya Ushindani (FCC) kwa ajili ya kupeleka malalamiko yao na kupinga ongezeko la bei ya umeme.
Maandamano hayo yanatarajia kuanzia Ofisi za chama hicho Ilala, kuanmzia saa tatu asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi, Bw. Faustine Sungura, alisema wamepata kibali cha kufanya maandamano hayo kutoka Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Saalam.
Alisema katika malalamiko wanayoyapeleka, kuna hoja kuu nane ambazo hawezi kuzitaja hadi zijibiwe na tume.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa kama amepata barua ya kuomba kibali cha maandamano hayo alisema hana taarifa hizo.
No comments:
Post a Comment